Washambuliaji wavamia kambi ya kijeshi Nigeria na kuua wanne
14 Mei 2025Jeshi nchini Nigeria limesema washambuliaji wenye silaha wamevamia kambi moja ya kijeshi kaskazini mashariki mwa Nigeria na kuwaua wanajeshi wanne na kuwachukua wengine mateka. Shambulio hilo limetokea siku moja baada ya shambulizi kama hilo lililowaua wanajeshi wanne pia.
Afisa mmoja wa kijeshi ameliambia shirika la habari la AFP kwamba wanamgambo wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu tawi la magharibi mwa Afrika, kwa kifupi, ISWAP, walivamia kambi ya kijeshi ya Rann mapema alfajiri katika jimbo la Borno, karibu na mpaka na Cameroon.
Soma zaidi: Mataifa ya Sahel kuunda muungano wa kupambana na wanamgambo wa kijihadi
Kundi hilo pamoja na lile la Boko Haram yamezidisha mashambulizi kwenye kambi za kijeshi katika wiki za hivi karibuni.
Takriban watu 100 wakiwemo wanajeshi wameuawa katika mashambulizi mbalimbali ya wanamgambo hao kaskazini mashariki mwa nchi hiyo mwezi Aprili.