Warohingya wataka wahakikishiwe usalama kurudi kwao
25 Agosti 2025Kumbukumbu hiyo ilifanyika mchana wa Jumatatu (Agosti 25) kwenye uwanja wa Kutupalong katika wilaya ya Cox's Bazar iliyo kusini mashariki mwa Bangladesh, huku waandamanaji wakibeba mabango yanayosomeka "Maisha ya kiukimbizi hayapaswi kuendelea" na "Kurejea nyumbani ni suluhisho pekee."
Waandamanaji hao walikusanyika kukumbuka kile kiitwacho "Siku ya Mauaji ya Kimbari ya Rohingya ," ambayo hukumbukwa kila tarehe 25 Agosti kuwatambuwa maelfu ya jamii hiyo ya Kiislamu waliouawa na kuangamizwa katika taifa lao la Myanmar, ambalo hadi sasa haliwatambui kuwa raia halali.
"Tunataka kurejea Arakan. Tunataka haki kwa mauaji ya kimbari dhidi yetu yaliyofanyika mwaka 2017. Wazazi, kaka, dada, marafiki na wazee waliteketezwa kwa moto na kukatwa kwa mapanga. Tulikimbilia nchi hii kwa sababu hatukuweza kuhimili mateso yale. Lakini hatutaki maisha haya ya ukimbizi. Tunataka kurudi nchini kwetu." Mmoja wa waandamanaji hao, Mohammad Anas, mwenye umri wa miaka 28, aliyasema hayo huku akilia.
Bangladesh yataka jumuiya ya kimataifa iwarejeshe Warohingya
Wakati huo huo, kiongozi wa mpito wa Bangladesh, Mohammad Yunus, aliitolea wito jumuiya ya kimataifa kutekeleza mpango wa kuwahakikishia wakimbizi hao wanarejea makwao salama usalimini.
Akizungumza kwenye kongamano la siku tatu lililoanza Jumatatu (Agosti 24) kwenye eneo hilo la Cox's Bazaar, mshindi huyo wa Tuzo ya Amani ya Nobel alisema uhusiano kati ya Warohingya na nchi yao ya asili hauwezi kuvunjwa na kwamba haki yao ya kurudi lazima isimamiwe kikamilifu, akisisitiza kuwa nchi yake haina tena nguvu za kiuchumi kuendelea kuwahudumia wakimbizi hao.
"Tulionesha huruma na tukawatendea wanaadamu wenzetu utu wakati wa nakama kubwa iliyojiri kwao, lakini hatuwezi tena kuendelea kukaa kimya juu ya hali yao ndugu zetu Warohingya. Kwa hivyo, tunaiomba jumuiya ya kimataifa kuchukuwa hatua za pamoja kuwazuwia watawala wa kijeshi wa Myanmar na jeshi la Arakan kuwashambulia Warohingya. Utawala wa kweli wa jumuiya ya kimataifa unahitajika muda huu kuliko wakati mwengine wowote hapo nyuma." Alisema Yunus.
Mnamo mwezi Agosti 2017, jeshi la Myanmar lilianzisha kampeni kubwa ya ukandamizaji kwenyejimbo la Rakhine , nyumbani kwa mamilioni ya Waislamu wa jamii ya Rohingya, kwa madai ya kukabiliana na mashambulizi dhidi ya vituo vyake.
Kiwango cha ukandamizaji na ukatili huo kilipelekea tuhuma za mauaji ya kimbari kutoka jumuiya ya kimataifa, ukiwemo Umoja wa Mataifa.
Reuters, dpa, AFP