Wapinzani wa Urusi wazuiwa viza Ujerumani?
18 Agosti 2025Takribani Warusi na Wabelarusi 300 wanaweza kujikuta wakizuiwa kupata vibali vya kuingia na kuishi Ujerumani baada ya uamuzi wa serikali mjini Berlin kusitisha programu yake ya viza kwa sababu za kibinaadamu mwishoni mwa Julai.
Kwa mujibu wa mradi wa Ark uliozinduliwa mnamo Machi 2022 kuwasaidia Warusi wanaoikimbia ukandamizaji wa mamlaka za Urusi, viza za watu hao zilikuwa zimeshaidhinishwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani, lakini Wizara ya Mambo ya Ndani imezuia kutolewa.
Wengi wa Warusi walioathirika na uamuzi huo ni wale walioikimbia nchi yao kutokana na upinzani wao dhidi ya vita vya Ukraine.
Kifungo kwa mchoro wa mtoto
Mmoja wao nji Alexei Moskalev, ambaye alitiwa hatiani nchini mwake baada ya binti yake kuchora mchoro unaonesha Urusi ikirusha makombora kuelekea Ukraine, huku mama akiwa ameshimama mbele ya mtoto akijaribu kumkinga mtoto huyo.
Moskalev alifungwa kifungo cha miaka miwili na binti yake, Masha, alipelekwa kituo cha mayatima, naye akaikimbia Urusi mwezi Oktoba 2024 mara tu baada ya kumalizika kutumikia kifungo chake, akihofia kukamatwa tena kama alivyokuwa ametishiwa na maafisa wa usalama wa Urusi.
Anton K. aliondoka Urusi mwanzoni mwa uvamizi wa nchi yake dhidi ya Ukraine. Mwandishi na mwanaharakati huyo alikuwa akiandikia magazeti yaliyobadikwa jina la mawakala wa kigeni na mamlaka za Urusi.
Baada ya kukamatwa akiachiliwa mara kadhaa, alikimbilia mojawapo ya mataifa ya Jumuiya ya Madola Huru (CIS) inayozijumuisha Armenia, Azerbaijan, Belarus, Kazakhstan, Kyrgyzstan, Tajikistan, Turkmenistan na Uzbekistan.
Hatari ya kurejeshwa Urusi
Mwanasheria Anastasia Burakova, mwanzilishi wa mradi wa Ark, aliiambia DW kwamba ni "hatari kwa wapinzani wa Kremlin kukaa kwenye mataifa hayo kwa muda mrefu, kwani wakati wowote wanaweza kukamatwa na kurejeshwa Moscow, ikiwa Urusi itataka hivyo."
Kwa mujibu wa Burakova, kumekuwa na majaribio kadhaa ya aina hiyo nchini Armenia, na mengine yalifanikiwa nchini Krygyzstan, ambapo waliotekwa waliishia kwenye magereza ya Urusi.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ujerumani iliiambia DW kwamba makubaliano ya vyama vinavyounda serikali ya mseto yalijumuisha azma ya kuzifuta programu za viza kwa wingi kadiri itakavyowezekana na kwamba kwa sasa wanatathmini jinsi ufutaji huo utakavyokuwa unatekelezwa.
Wizara hiyo ilisema usitishwaji wa sasa wa programu ya viza kwa sababu za kibinaadamu unalenga kulinda maslahi ya kisiasa ya Ujerumani kwa mujibu wa sheria za nchi.
Kufikia mwezi huu wa Agosti kuna watu 1,043 wanaotambuliwa kuwa wafungwa wa kisiasa ndani ya Urusi na kwa mujibu wa mtandao huru wa habari unaofanya kazi zake nje ya nchi hiyo, The Bell, kiasi cha watu 700,000 wameikimbia Urusi tangu kuanza kwa vita vya Moscow dhidi ya Kiev.