Wapiganaji wa PKK waanza kuweka chini silaha
11 Julai 2025Hatua hiyo inatajwa kuwa muhimu katika mchakato mpana wa amani kati ya PKK na taifa la Uturuki. Usalimishaji huo wa silaha ulifanyika katika pango la Jasana, eneo la kihistoria karibu na mji wa Dokan, kwa kuwashirikisha wapiganaji wapatao 30 wa PKK, kulingana na shirika la habari la ANF linaloshirikiana na PKK. Taarifa ya PKK imesema hatua hiyo ni ishara ya nia njema ya kuendeleza mchakato wa amani na kuitikia wito wa kiongozi wao Abdullah Öcalan aliyeko gerezani.
Walitangaza kuachana na mapambano ya kutumia silaha na badala yake kujihusisha kisiasa, wakithibitisha kujitolea kwao kupigania "uhuru, demokrasia, na ujamaa kupitia njia za kisheria na kidemokrasia. Tukio hilo linafuatia wito wa Öcalan uliotolewa kwa njia ya video mnamo Juni 19 na taarifa ya awali mnamo Februari, akiwataka wanamgambo wa PKK kuweka chini silaha na kukumbatia njia ya kisiasa. Serikali ya Uturuki imekaribisha uamuzi huo na kuiita hatua "halisi na isiyoweza kurudishwa nyuma" ambayo inaweza kufungua njia ya mustakabali wa amani na kidemokrasia, usio na ghasia na ugaidi.