Wapatanishi wa kimataifa wataka misaada ifikie raia wa Sudan
21 Agosti 2025Wito huo umetolewa kufuatia kuzorota kwa hali ya kibinadamu nchini humo, ambapo mamilioni ya watu wanakabiliwa na njaa na ukosefu wa huduma za kimsingi zikiwemo za afya.
Wamezihimiza pande zote zinazohasimiana; jeshi la serikali na wanamgambo wa RSF kulinda raia na kuruhusu misaada ya kibinadamu kwa watu wanaoihitaji. Muungano huo wa ALPS unajumuisha Marekani, Saudi Arabia, Uswisi, Umoja wa Falme za Kiarabu, Misri, Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.
Zaidi ya watu milioni 12 wamekimbia makazi yao nchini Sudan tangu kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe mnamo mwezi Aprili 2023, vilivyosababishwa na mvutano wa madaraka kati ya kiongozi wa kijeshi Abdel-Fattah al-Burhan na naibu wake Mohamed Hamdan Daglo, ambaye anaongoza kikosi cha wanamgambo cha RSF.