Wapalestina zaidi ya 30 wauawa Ukanda wa Gaza
30 Juni 2025Idara inayoshughulikia usalama wa raia kwenye Ukanda wa Gaza imesema watu 35 wameuawa na vikosi vya Israel siku ya Jumapili ikiwemo 11 waliouawa karibu na vituo viwili vya kugawa misaada ya kiutu vinavyosimamiwa na wakfu ulioanzishwa kwa uungaji mkono wa Israel na Marekani.
Shirika la Habari la Palestina, WAFA, likinukuu mashuhuda ambao hawakutajwa majina, limesema watu hao wameuliwa karibu na vituo viwili vya kutoa misaada kimoja katikati mwa Gaza na kingine kwenye mji wa kusini wa Rafah.
Wakfu unaosambaza misaada hiyo umesema umekuwa ukigawa mahitaji bila tukio lolote na umelituhumu kundi la Hamas linalotawala Gaza kuwa chanzo cha kuvuruga usambazaji misaada.
Mbali ya ripoti za mauaji hayo karibu na vituo vya misaada, mashuhuda wengine wamesema watu 11 wamepoteza maisha baada ya nyumba ya nyumba maakazi kushambuliwa na kombora la Israel kwenye eneo la Jabalia kaskazini mwa Gaza.
Taarifa hizo hazikuweza kuthibitishwa na vyanzo huru vya habari lakini Jeshi la Israel lilipoulizwa kuhusiana na mashambulizi hayo yanayowalenga raia limesema linachunguza madai hayo.
Israel yaamuru maelfu ya Wapalestina kuondoka kaskazini mwa Gaza
Vifo hivyo vilivyoripotiwa vimetokea wakati maelfu ya familia za Wapalestina zimeyahama makaazi yao kaskazini mwa Gaza na eneo la Jabalia kuitikia amri iliyotolewa na jeshi la Israel.
Jeshi hilo liliamuru watu kukusanya waliacho nacho na kuondoka maeneo hayo ili kupisha mashambulizi iliyotaka kuyafanya.
Tangu kuzuka kwa vita miezi 20 iliyopita, Wapalestina wanaoishi kwenye ardhi hiyo ndogo ya Gaza wamekuwa wakiamriwa kuyahama maeneo yao kila wakati, wakiondoka na vitu vichache na pale wanaporejea hukuta karibu kila kitu kimeharibiwa.
Mmoja ya wale waliotikia amri ya jeshi la Israel hapo jana Jumapili Sarian Badrah amesema
"Kama unavyoona, hakuna unga, hakuna mahitaji, hakuna chakula wala maji. Tunahama kutoka eneo moja hadi jingine. Kosa letu ni lipi, Mungu wangu? Tumefanya nini kustahili haya? Tunateseka kwa maumivu, sote tunaumwa. Tunaomba, mtu atutafutie suluhisho la haya". amesema Sarian Badrah, mmoja ya wale waliotikia amri ya jeshi la Israel ya kuondoka nyumbani kwake.
Israel yasema vita vinaendelea licha ya shinikizo la Marekani
Hayo yakijiri, viongozi wa Israel hawaoneshi dalili ya kumalizika vita hivyo vilivyozuka Oktoba 7 2023, pale kundi la Hamas lilipoivamia Israel na kuwaua watu wapatao 1,200.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema bado wamedhamiria kulishinda kundi la Hamas na kuwarejesha mateka wa nchi hiyo walio mikononi mwa kundi hilo.
Hata hivyo shinikizo linaongezeka kwa utawala mjini Tel Avivkuvikisha mwisho vita hivyo. Rais Donald Trump wa Marekani, hapo jana alitoa rai ya kufikiwa mkataba wa kumaliza vita. Aliandika kwenye ukurasa wa mtandao wake wa kijamii wa Truth Social akihimiza hilo na kuashirikia litasaidia kuwaokoa mateka wa Israel walio hai.
Ijumaa iliyopita Trump aliashiria mktaba unaweza kufikiwa ndani ya wiki hii. Waziri Mkuu Netanyahu anatazamiwa kusafiri kwenye Washington mnamo wiki zijazo pengine kwa lengo la kujadiliana na Trump hatma ya vita vya Gaza.
Hata hivyo matumaini miongoni mwa Wapalestina ni madogo ikitiliwa maanani kuwa msimamo serikali ya Israel ni kuendeleza vita hadi kutimiza lengo wanalosema kuwa "kulitokomeza kabisa kundi la Hamas".