Zaidi ya Wapalestina 20 wauwawa wakisubiri misaada Gaza
24 Juni 2025Mamlaka za Ukanda wa Gaza zimearifu kuwa watu zaidi ya 20 waliokuwa wakisubiri chakula wameuwawa katika tukio la mapema Jumanne. Msemaji wa idara ya ulinzi wa raia katika ukanda huo Mahmud Bassal amesema watu wengine 150 wamejeruhiwa.
Mmoja wa Wapalestina waliokuwa wakisubiri misaada aliyejitambulisha kwa jina moja la Maha amesema, "Nilikuja hapa kwakuwa walisema kutakuwa na malori ya misaada. Kama unavyoona sikuja peke yangu, nilikuja na watu wengine wote. Ninataka nikuambie, idadi ya wanawake hapa ni kubwa kuliko wanaume. Kwanini wamekuja? Wamekuja tu kupata chochote kwa ajili ya kuwalisha watoto wao. Hakuna kingine cha ziada."
Maelfu ya wapalestina wamekuwa wakikusanyika kila siku wakiwa na matumaini ya kupata chakula baada ya vita vya zaidi ya miezi 20 lakini wamekuwa wakilengwa na mashambulizi ya Israel.
Umoja wa Mataifa walaani Israel kutumia njaa kama silaha
Kutokana na hali mbaya ya upatikanaji wa chakula kwenye ukanda huo, Umoja wa Mataifa umeikosoa vikali Israel kwa kuitumia njaa kama silaha na kwamba huo ni uhalifu wa kivita.
Katika taarifa iliyotolewa Jumanne, Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa imelitaka jeshi la Israel liache kuwafyatulia risasi watu wanaojaribu kupata chakula.
Taasisi ya kutoa misaada inayoungwa mkono na Marekani na Israel "Gaza Humanitarian Food Foundation" ilianza kugawa chakula Ukanda wa Gaza Mei 26 baada ya Israel kuzuia kabisa usambazaji wa chakula katika eneo kwa zaidi ya miezi miwili na kuibua tahadhari ya njaa kali. Mashirika makubwa ya Umoja wa Mataifa yamekataa kushirikiana na taasisi hiyo kutokana na wasiwasi kuwa imeundwa kwa maslahi ya jeshi la Israel.
Soma zaidi: Israel yaendeleza mashambulizi Gaza
Katika hatua nyingine kiongozi wa upinzani nchini Israel Yair Lapid ametoa wito wa kusitishwa kwa vita kati ya jeshi la nchi yake na wanamgambo wa kundi la Hamas katika Ukanda wa Gaza.
Ameyasema hayo kupitia ukurasa wake wa X muda mfupi baada ya Israel kutangaza kuwa imekubali kusitisha vita na Iran.
Hayo yanaendelea wakati ndugu wa mateka waliosalia Gaza wakiishinikiza pia serikali yao iiingie katika mazungumzo ya haraka yatakayowarejesha nyumbani jamaa zao na kumaliza vita.