Wapalestina wana hofu juu ya Israel kujenga makazi mapya
15 Agosti 2025Waziri wa fedha wa Israel Bezalel Smotrich, anayeegemea mrengo mkali wa kulia amesema ujenzi wa makazi hayo mapya katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Israel utaendelea. Wapalestina na makundi ya kutetea haki za binadamu yana wasiwasi kwamba mradi huo unaolenga kuligawa eneo la Ukingo wa Magharibi katika sehemu mbili utavuruga mipango ya kuundwa kwa taifa huru la Palestina.
Tamko la Waziri wa Fedha wa Israel limekemewa na nchi nyingi, zikiwemo Australia, Uingereza, Ufaransa na Canada ambazo zinasema zinapanga kuitambua Palestina ifikapo mwezi Septemba, katika Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Mpango wenye utata, wa miaka mingi wa ujenzi kwenye kipande cha ardhi katika eneo la mashariki mwa Jerusalem kilichopewa jina la E1, umekuwa unazingatiwa na Israel kwa zaidi ya miongo miwili, eneo hilo lina utata kwa sababu ni mojawapo ya maeneo ya mwisho yaliyo na historia ya mipaka ya kijiografia kuhusiana na miji mikogwe na maarufu ya Ukingo wa Magharibi, Ramallah na Bethlehem.
Kulingana na mkuu wa baraza la kijiji cha al-Jahalin, Dahoud al-Jahalin, eneo la E1 ni nyumbani kwa karibu watu 7000 wa jamii ya Bedouin na kwamba mradi huo ni pigo la mwisho katika ndoto ya kuzaliwa kwa taifa la Palestina.
Dahoud al-Jahalin amesema ni muhimu kwa jumuiya ya Kimataifa kuchukua hatua na kutekeleza wajibu wa kuizuia serikali ya Israel kwa kusimamisha utekelezaji wa mpango huu.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa mamlaka ya Israel kusitisha mara moja uendelezaji wa mipango ya ujenzi wa makazi katika eneo la E1 la Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.
Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric, amewaambia waandishi wa habari kwamba Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema makazi ya Waisraeli katika Ukingo wa Magharibi ikiwa ni pamoja na mji wa Jerusalem Mashariki, yanakiuka sheria za kimataifa.
Ujerumani imetoa wito kwa serikali ya Israel wa kusitisha ujenzi wa makazi mapya katika Ukingo wa Magharibi. Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani kwenye taarifa yake imesema inapinga kabisa hatua ya serikali ya Israel ya kuidhinisha ujenzi wa nyumba mpya zipatazo 3,401 kwa ajili ya walowezi wa Kiyahudi katika Ukingo wa Magharibi imesema ujenzi huo unakiuka sheria za kimataifa na maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani imesema hatua kama hizo zinatatiza hatua za kuelekea kwenye makubaliano ya kuundwa nchi mbili.
Vyanzo: AP/RTRE