Wapalestina wakosoa vikali wazo la Trump la "kusafisha Gaza"
27 Januari 2025Baada ya miezi 15 ya vita, Trump amesema Gaza imekuwa kile alichokiita "eneo la ubomoaji", akiongeza kuwa amezungumza na Mfalme Abdullah II wa Jordan kuhusukuwahamisha Wapalestina nje ya eneo hilo.
Ofisi ya Rais Abbas iliyoko Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Israel, imepinga na kulaani mipango yoyote inayolenga kuwahamisha Wapalestina kutoka Gaza. Imesema Wapalestina hawataitelekeza ardhi yao na maeneo matakatifu. Bassem Naim, mwanachama wa ofisi ya kisiasa ya Hamas amesema Wapalestina watazuia miradi ya aina hiyo kama tu walivyofanya katika miongo mingi iliyopita. Kundi la Islamic Jihad linalopigana pamoja na Hamas huko Gaza limesema wazo la Trump ni la kusikitisha na linahimiza uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu.
Pendekezo hilo pia limepingwa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu. Waziri wa Mambo ya Nje wa Jordan Ayman Safadi amesema uamuzi wao wa kupinga uhamishwaji wa Wapalestina ni thabiti na hautabadilika. Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri ilisema inakataa ukiukwaji wowote wa "haki zisizoweza kuguswa" za Wapalestina, ikiwa ni pamoja na "kukaa au kunyakua ardhi, au kwa kuondolewa kwa ardhi ya watu wake kwa njia ya uhamisho, au kuhimiza uhamisho au kung'olewa kwa Wapalestina kutoka ardhi yao, iwe kwa muda mfupi au kwa muda mrefu".