Wapalestina wachoshwa kuhamishwa katika makazi yao
3 Aprili 2025Hivi sasa Israel ambayo ilianzisha tena mashambulizi yake dhidi ya Gaza imetoa amri ya raia chungunzima kuondoka kwenye maeneo inayolenga kuyasambaratisha. Wengi wanajikuta wanabeba vitu vichache tu wakitafuta sehemu mpya ya kujibanza kukwepa mapigano.
Wapalestina hao wanasema wamechoshwa na hali hiyo ya kuhamishwa kwa ghafla na kila mara. Walipotakiwa na jeshi la Israel kuondoka eneo la kaskazini mwa Gaza la Jabaliya mnamo Machi 19, Ihab Suliman na familia yake walifanikiwa tu kubeba chakula kidogo na mablanketi kabla ya kuanza safari yao kuelekea kusini mwa Ukanda huo.
Ilikuwa mara yao ya nane kulazimika kuyahama makazi yao katika kipindi cha miezi 18 ya vita. Profesa huyo wa zamani wa chuo kikuu anasema maisha yao kwa sasa hayana furaha na hayatofautiani na kifo.
Suliman ni miongoni mwa maelfu ya Wapalestina waliolazimika kuyakimbia makazi yao tangu Israel ilipovunja makubaliano ya usitishaji mapigano mnamo Machi 18 na kuanza wimbi jipya la mashambulizi ya angani na ardhini.
Wakihofia kuanza upya maisha yao, baadhi ya Wapalestina wamekuwa wakipuuza miito na maagizo ya kuondoka katika makazi yao bila kujali ikiwa uamuzi wao huo unaweza kuhatarisha maisha yao.
Rosalia Bollen, mtaalamu wa mawasiliano wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia watoto UNICEF anasema kuwa vita hivi vimemchosha kila mtu huko Gaza ikiwa ni pamoja na watoto na wazazi wao ambao wamechoka si tu kimwili bali kiakili pia.
Soma pia: Uingereza yasema haiungi mkono mpango wa Israel kwa Gaza
Mwezi uliopita, Israel ilichukua uamuzi wa kuzuia chakula, mafuta na vifaa vyote muhimu kuingia Gaza, huku mashirika ya misaada yakitahadharisha kuhusu hali mbaya ya kibinaadamu kutokana na uhaba mkubwa wa mahema na vifaa vingine vya malazi ili kuwasaidia watu waliohamishwa hivi karibuni.
Mapema siku ya Jumanne, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP lililazimika kufunga viwanda vyake vyote vya kuoka mikate huko Gaza, ambavyo vinategemewa na maelfu ya raia kwa sababu tu ya kuishiwa unga wa ngano.
Amri za jeshi la Israel zapelekea raia wengi kulazimika kuhama bila chochote
Amri za kuwahamisha Wapalestina zinatolewa na Israel sasa zinayahusu maeneo makubwa zaidi ya Ukanda wa Gaza, ikiwa ni pamoja na mjini kati na miji ya kaskazini, sehemu za miji ya kusini ya Khan Younis, na karibu eneo zima la Rafah na vitongoji vyake. Kulingana na makadirio ya hivi punde ya Umoja wa Mataifa, kufikia Machi 23, zaidi ya watu 140,000 walikuwa wamehamishwa tena tangu kuvunjika kwa makubaliano ya usitishaji mapigano.
Kila wakati familia zinapohamishwa wakati wa vita, huondoka mikono mitupu na kuacha mali zao na kulazimika kuanza upya maisha yao kwa kutafuta kwanza makazi kisha chakula na maji safi. Suliman anasema kutokana na uhaba wa mafuta, usafiri umekuwa mgumu na wenye mateso makubwa. Kumekuwa kukishuhudiwa pia mlolongo wa watu wakisubiri msaada wa chakula.
Soma pia:Israel inatanua operesheni Gaza ili kuteka 'maeneo makubwa'
Wakati makubaliano ya usitishaji mapigano kwa miezi miwili yalipoanza kutekelezwa mwezi Januari huko Gaza, maelfu ya Wapalestina walimiminika mitaani kuanza kurejea katika makazi yao bila kujali kuwa nyumba zao ziliharibiwa. Waliweka mahema karibu na vifusi na walifarijika tu kuwa makwao.
Wapalestina hao walikuwa na matumaini ya kwamba huo ndio ungelikuwa mwisho wa kuhamishwa kila mara, lakini sasa wamejikuta wakirejeshwa kwenye madhila ya kutangatanga ambayo yamewakumba Wapalestina zaidi ya milioni 2 tangu kuanza kwa vita hivyo.
(Chanzo: AP)