Wapalestina 52,400 wameuawa ndani ya miezi 18 iliyopita Gaza
1 Mei 2025Mashambulizi ya angani yanayoendelea kufanywa na Israel katika Ukanda wa Gaza yameua maelfu ya raia, huku hali ya kibinadamu ikizidi kuwa mbaya. Katika saa 24 zilizopita pekee, watu 35 waliuawa na 109 kujeruhiwa.
Mashambulizi hayo yamekuwa ya kila siku tangu Israel ilipoanzisha tena operesheni za kijeshi mnamo Machi 18, ikivunja usitishaji wa mapigano wa miezi miwili.
Soma pia: Israel yashambulia jengo la hospitali kuu Gaza
Tangu wakati huo, Wapalestina 2,308 wameuawa na zaidi ya 5,900 kujeruhiwa.
Katika shambulio lililoripotiwa Jumatano na shirika la habari la WAFA, watu wasiopungua 12 waliuawa kwenye kambi ya wakimbizi ya Nuseirat, wakiwemo watoto, huku mashambulizi mengine yakiripotiwa Jabalia na Khan Younis.
Misaada ya kibinadamu imepungua pakubwa Gaza
Wakati hayo yakiendelea, Umoja wa Mataifa kupitia shirika lake la misaada ya kibinadamu (OCHA) umeonya kuwa misaada ya dharura imefikia ukingoni.
Hospitali nyingi zimefungwa, vifaa vya kujifungulia kinamama vimeisha, na visa vya utapiamlo kwa watoto wachanga vinaongezeka kwa kasi. Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Farhan Haq, amesema kuwa majiko zaidi ya kijamii yamefungwa Gaza kutokana na ukosefu wa vifaa na mahitaji.
"Wakati zuwio kamili la uingizaji wa mahitaji yoyote Gaza likikaribia miezi miwili, akiba za mahitaji muhimu zinaendelea kuisha au zimeisha kabisa. Hali hii imewaacha watu zaidi ya milioni 2 wakikabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula, maji, makazi, dawa na vifaa vingine vya msingi. Washirika wetu wameripoti kuwa majiko zaidi ya kijamii yamefungwa wiki hii, na hakuna hata hema moja lililobaki la kugawa."
Katika maeneo kama Deir al-Balah na Nuseirat, mamia ya raia hukusanyika kila siku kwenye majiko ya misaada kupata mlo mmoja tu. Hata hivyo, majiko hayo yanakaribia kufungwa kutokana na ukosefu wa chakula na mafuta. Wapishi wa misaada wanasema majiko madogo tayari yamefungwa na waliobaki wanategemea machache ya pamoja.
Katika taarifa nyingine, shirika la Hilali Nyekundu la Palestina limesema mhudumu wake Asaad al-Nsasrah, ameachiliwa na Israel pamoja na wafungwa wengine tisa kutoka Gaza.
Soma pia: Jeshi la IDF kuchunguza vifo vya wafanyakazi wa misaada Gaza
Al-Nsasrah alikamatwa Machi 23, siku ambayo wanajeshi wa Israel waliwaua madaktari wanane wa Hilali Nyekundu, waokoaji sita wa serikali ya Hamas, na mfanyakazi mmoja wa Umoja wa Mataifa, na kisha miili yao kufukiwa katika shimo la pamoja na wanajeshi hao wa Israel.
Kaburi hilo la pamoja lilifikiwa na waokoaji wiki moja baadaye. Zaidi ya wahudumu 1,000 wa afya wameuawa tangu vita kuanza.
Balozi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa, Riyad Mansour, ameeleza kuwa alizuiwa na maafisa wa Israel kwa saa tano na kukataliwa kuingia Ramallah kwa ajili ya mkutano. Amesema kitendo hicho ni sehemu ya mkakati wa adhabu ya pamoja dhidi ya Wapalestina na kukanusha haki yao ya kuwa taifa huru.
Katika muktadha mpana wa ukanda huo, Uingereza ikishirikiana na Marekani imefanya mashambulizi ya anga dhidi ya waasi wa Kihouthi nchini Yemen, karibu na mji wa Sanaa. Mashambulizi hayo ni sehemu ya "Operation Rough Rider", ambayo inalenga vituo vya utengenezaji wa droni zinazotumika kushambulia meli katika Bahari Nyekundu na Ghuba ya Aden.
Mashambulizi hayo yamesababisha vifo vya raia, wakiwemo wahamiaji wa Kiafrika waliouawa katika shambulio lililolenga gereza hivi karibuni.
Katika hatua ya kuongeza shinikizo, Waziri wa Ulinzi wa Marekani ametuma ujumbe wa wazi kwa Iran kwenye mtandao wa X, akiitishia kutokana na msaada wake kwa waasi wa Houthi.