Mashambulizi ya Israel yauwa watu 25 Gaza
8 Aprili 2025Shambulio moja liliilenga nyumba kwenye mji wa Deir al Balah, ambapo watu 11 wameuwawa wakiwemo watoto watano. Mama wa mmoja wa watoto waliouwawa katika shambulio hilo aliyefahamija kwa jina Jana ameelezea namna tukio hilo lilivyokuwa akisema, "tulikuwa tumelala, hatukufanya kosa lolote na ghafla nyumba ikatuangukia. Mtoto wangu alikuwa amelala pembeni yangu, walikuwa kando yangu lakini wamekwenda."
Katika Ukingo wa Magharibi, Wizara ya Afya imesema wanajeshi wa Israel wamemuuwa mwanamke mwenye miaka 30 katika mji wa Salfit Jumanne baada ya kile jeshi hilo lilichokitaja kuwa jaribio la shambulio la kisu.
Kwa upande wake Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameyalaani mashambulizi ya Israel dhidi ya Wapalestina, akiyataja kuwa ni uhalifu wa kivita. Ameyataja na kuyakosoa vikali matukio kadhaa likiwemo la jeshi la Israel kuilifyatulia risasi gari la wagonjwa na mauaji dhidi ya wahudumu wa afya. Akizungumza mjini Ankara, Erdogan amesema serikali yake itaendelea kufanya juhudi za kidiplomasia ili kuzuia mapigano katika Ukanda wa Gaza.
Mashambulizi hayo yanajiri wakati, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameutembelea mji wa bandari wa El Arish wa Misri, ambao ni kituo muhimu cha kupitisha misaada inayopelekwa Ukanda wa Gaza. Ameifanya ziara hiyo kwa madhumuni ya kutoa wito kwa Israel kufungua vivuko vya kupitisha misaada na kuitaka iruhusu misaada ya kiutu kuingia katika ukanda huo.
Mahakama ya Israel yaanza kusikiliza kesi ya kupinga kusimamishwa kwa mkuu wa usalama
Katika hatua nyingine, mahakama ya juu ya Israel imeanza kusikiliza kesi ya pingamizi dhidi ya uamuzi wa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu wa kumfuta kazi mkuu wa shirika la usalama wa ndani Shin Bet, Ronen Bar. Maandamano ya raia ya kuipinga hatua hiyo yameshuhudiwa ndani na nje ya mahakama hiyo, hali iliyomlazimu jaji Yitzhak Amit kusimamisha kwa muda kusikilizwa kwa kesi hiyo.
Mwezi uliopita, Netanyahu alitangaza kuwa serikali yake kwa sauti moja imeidhinisha kumfuta kazi Bar kutokana na kukosa imani naye na kumtaka aondoke kwenye nafasi yake ifikapo Aprili 10.