Wapalestina 21 wauwawa
24 Juni 2025Shirika la ulinzi wa raia katika Ukanda wa Gaza limesema kuwa wanajeshi wa Israel wamewaua watu 21 leo Jumanne, waliokuwa wakisubiri msaada wa chakula karibu na kituo cha usambazaji katikati mwa mji huo.
Kwa mujibu wa mashuhuda na maafisa wa eneo hilo, watu hao walikuwa wamekusanyika kwa matumaini ya kupokea mgao wa misaada wakati mashambulizi yalipotokea.
Wakati huo huo, familia za raia wa Israel wanaoshikiliwa mateka na kundi la Hamas katika Ukanda wa Gaza zimeitaka serikali yao kusitisha mara moja mashambulizi dhidi ya Gaza, wakitoa mfano wa makubaliano ya kusitisha vita kati ya Iran na Israel yaliyotangazwa hivi karibuni.
Katika tamko la pamoja lililotolewa na Jukwaa la Familia za Mateka na Watu Waliopotea, familia hizo zimetaka mazungumzo ya dharura yaanze haraka ili kuhakikisha kuachiliwa kwa mateka wote na kusitishwa kabisa kwa mapigano, kama ilivyofanyika kati ya Israel na Iran.