Wapalestina 120 wauawa na jeshi la Israel ukanda wa Gaza
16 Mei 2025Israel imesema hatua ya kuzuia misaada kuingia katika Ukanda wa Gaza inalenga kuishinikiza Hamas kufikia makubaliano na kuwaachia mateka wa Israel inaoendelea kuwashikilia, lakini kundi hilo limesisitiza kwamba kurejeshwa kwa misaada ya kibinadamu katika eneo hilo lililoharibiwa na vita ni "hitaji la msingi" kwa mazungumzo ya amani.
Afisa wa ngazi za juu kutoka kundi la Hamas Basem Naim, amesema misaada ya msingi ya chakula na madawa haipaswi kuchukuliwa kama sharti la Israel kwa sababu hizo ni haki za binadamu.
Mashirika ya umoja wa mataifa yameonya mara kadhaa dhidi ya wimbi la majanga katkaukanda wa Gaza ambapo ukosefu wa chakula, maji safi na salama, madawa na mafuta havipatikani kwa urahisi sasa.
Shirika la afya ulimwenguni WHO limesema kwamba hospitali ya kutibu magonjwa ya saratani, moyo na ambayo ndiyo ilikuwa imebaki ikifanya kazi imesitisha shughuli zake za matibabu kutokana na mashambulizi ya Israel, amesema mtetezi wa umoja wa mataifa Francesca Albanese.
"Tunatazamia kutafuta suluhu ya Ukanda wa Gaza"
Akizungumza katika ziara yake huko mashariki ya kati Rais Donald Trump wa Marekani amesema kwa mara nyingine tena kwamba Marekani italichukua na kulidhibiti eneo la Gaza huku akirejelea kauli zake zenye utata kwamba Marekani italijenga na kuliendeleza upya eneo hilo.
"Tunakwenda kutatua baadhi ya changamoto mlizo nazo hapa kwa hakika na tunatazamia kutafuta suluhu ya Ukanda wa Gaza kwa sababu watu pale wanakufa kwa njaa, mambo mabaya kabisa yanaendelea kutokea pale", alisema Trump.
Kauli hii ya Trump imezua lawama zaidi kutoka kwa wapalestina na mashirika mbalimbali ya kutetea haki za binadamu. Jeshi la Israel limesema limefanya mashambulizi hayo kwa kutumia silaha nzito na kwamba litaendelea na operesheni hiyo.