Washirika wa Riek Machar wakamatwa, makazi yake yazingirwa
5 Machi 2025Sudan Kusini, taifa changa zaidi duniani, linaendelea kukumbwa na hali ya kisiasa isiyo tulivu, huku kukamatwa kwa viongozi wa ngazi ya juu hivi karibuni kukizua hofu ya kurejea kwa machafuko.
Mvutano uliongezeka Jumatano wakati vikosi vya usalama vilipomkamata Waziri wa Mafuta Puot Kang Chol na Naibu Mkuu wa Jeshi, Jenerali Gabriel Duop Lam, wote wakiwa washirika wa karibu wa Makamu wa Rais Riek Machar.
Jeshi la Ulinzi la Watu wa Sudan Kusini (SSPDF), linalomuunga mkono Rais Salva Kiir, pia lilizingira makazi ya Machar katika mji mkuu, Juba, jambo lililozidisha wasiwasi kuhusu mustakabali wa mkataba wa amani wa nchi hiyo.
Kukamatwa kwa viongozi hao kumetokea wakati wa hali ya kuzidi kwa machafuko katika jimbo la Upper Nile, ambapo jeshi linawatuhumu washirika wa Machar kwa kusaidia vikundi vya waasi, hususan kundi la White Army, ambalo linajumuisha wapiganaji wengi wa jamii ya Nuer.
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) umeripoti ongezeko la mapigano kati ya jeshi na "vijana wenye silaha" katika Kaunti ya Nassir, mapigano yaliyohusisha silaha nzito na kusababisha vifo na majeruhi kwa raia na askari.
Historia ya migogoro na utekelezaji wa polepole wa mageuzi
Uongozi wa Sudan Kusini umekuwa ukikumbwa na migawanyiko tangu taifa hilo lipate uhuru wake mwaka 2011. Uhasama kati ya Kiir na Machar ulisababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya 2013 na 2018, ambavyo viligharimu maisha ya takriban watu 400,000.
Vita hivyo vilimalizika kwa makubaliano ya kugawana madaraka, lakini utekelezaji wa vipengele muhimu vya mkataba, ikiwemo uundwaji wa katiba mpya, marekebisho ya sekta ya usalama, na uchaguzi wa kitaifa, bado haujakamilika.
Soma pia: Kiir aitisha mjadala wa kitaifa wa amani
Msemaji wa Machar, Pal Mai Deng, alikemea vikali kukamatwa kwa viongozi hao, akieleza kuwa hatua hiyo "inakwamisha" mkataba wa amani na inaweza kuusambaratisha kabisa. Alitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuingilia kati haraka ili kuzuia kurejea kwa mapigano ya wazi.
"Kitendo hiki kinahatarisha mkataba mzima wa amani. Tunatoa wito kwa wadhamini wa mkataba na washirika wa kimataifa kuingilia kati mara moja," alisema.
Wakati huohuo, Ter Manyang Gatwich, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Amani na Utetezi, alihimiza kuachiliwa mara moja kwa waliokamatwa, akionya kuwa kuendelea kwa mzozo huu kunaweza kuleta vita kamili.
Msimamo wa serikali na maoni ya kanda
Jumatatu, Rais Kiir alifanya mkutano wa ngazi ya juu, akiwemo Machar na Waziri wa Mafuta, kujadili hali ya usalama katika Upper Nile na kutuma vikosi vya ziada vya SSPDF katika eneo hilo.
Mamlaka ya Maendeleo ya Kiserikali (IGAD), jumuiya ya kanda yenye wanachama wanane, ilielezea "wasiwasi mkubwa" kuhusu ongezeko la ghasia, ikionya kuwa zinaweza kuhujumu maendeleo yaliyopatikana chini ya mkataba wa amani na kuzidisha hali mbaya ya kibinadamu.
Hii si mara ya kwanza Rais Kiir anatuhumiwa kuvuruga mkataba wa amani. Mwezi uliopita, aliwafuta kazi wawili kati ya makamu wake watano serikalini bila kushauriana na wadau wengine, hatua ambayo Machar aliieleza kuwa tishio kwa mkataba huo.
Uchaguzi uliopaswa kufanyika Desemba 2022 uliahirishwa kwa miaka miwili kwa sababu ya changamoto za kifedha na kiutendaji, jambo lililoongeza malalamiko juu ya ucheleweshaji wa mchakato wa kidemokrasia.
Changamoto zinazoikumba Sudan Kusini
Licha ya kuwa na akiba kubwa ya mafuta, Sudan Kusini bado inakabiliwa na umaskini mkubwa, huku mamilioni ya watu wakitegemea misaada ya kibinadamu.
Ufisadi, hali mbaya ya uchumi, na ghasia za kijamii zinaendelea kuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya nchi hiyo. Mvutano wa kisiasa wa hivi karibuni unaibua maswali zaidi kuhusu hatma ya mkataba wa amani na ikiwa nchi hiyo iko kwenye njia ya kurejea katika vita.
Kwa kuongezeka kwa shinikizo la kimataifa, macho yote yanaelekezwa kwa uongozi wa Sudan Kusini kuona ikiwa watafanikiwa kupunguza mvutano na kujitolea kutekeleza mkataba wa amani kwa ukamilifu. Rais Salva Kiir ametangaza kuwa Sudan Kusini haitarudi vitani, msemaji wa serikali alisema Jumatano.
Hatma ya wale waliokamatwa bado haijulikani, na iwapo mgogoro huu utasababisha mgawanyiko zaidi wa kisiasa au mazungumzo ya maridhiano itategemea jinsi viongozi wa ndani na jumuiya ya kimataifa watakavyoitikia hali hii katika wiki zijazo.