Wanamgambo wawauwa wanajeshi 20 Nigeria
26 Januari 2025Mmoja wa wanajeshi waliosalimika katika tukio hilo aliyeomba kutokutajwa jina kwa kuwa hana mamlaka ya kulizungumzia suala hilo kwa vyombo vya habari amesema walivamiwa ghafla mwishoni mwa juma, na licha ya wanajeshi kujaribu kulizima shambulio hilo walizidiwa nguvu. Msemaji wa jeshi la Nigeria hakupatikana kwa haraka kuuzungumzia mkasa huo.
Soma zaidi: Boko Haram yaua watu 37 katika shambulio la kigaidi Nigeria
Makundi ya wanamgambo ya Boko Haram na lile linalojiita dola la Kiislamu tawi la Afrika Magharibi ISWAP yanayoendesha shughuli zao katika jimbo la Borno yakilenga vikosi vya usalama na raia yamesababisha vifo vya maelfu ya watu na maelfu wengine wamelazimika kuyahama makazi yao.
Katika tukio jingine, mamlaka za Nigeria zimesema kuwa watu 18 wamekufa kutokana na ajali ya lori la mafuta katika jimbo la Enugu. Chanzo cha ajali hiyo kinaelezwa kuwa ni kufeli kwa breki hali iliyosababisha dereva kushindwa kulidhibiti lori na kuyagonga magari mengine 17 na kisha kuzua moto mkubwa. Ajali hiyo imetokea wiki moja baada ya lori jingine la mafuta kulipuka nchini humo na kusababisha vifo vya watu 98.