Wanamgambo wawateka abiria 450 wa treni nchini Pakistan
11 Machi 2025Haya ni kwa mujibu wa maafisa wa serikali. Katika taarifa yake, kundi linalotaka kujitenga la Jeshi la Ukombozi la Baloch (BLA) limesema kuwa watu wenye silaha walishambulia kwa mabomu njia ya reli na kuchukua udhibiti wa treni hiyo katika wilaya ya Sibi.
Afisa mmoja mkuu wa shirika la reli huko Quetta, Muhammad Kashif, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba zaidi ya abiria 450 wameshikiliwa mateka na wanamgambo hao.
Afisa mmoja wa polisi kutoka eneo linalopakana na Sibi, aliyezungumza kwa sharti la kutotambulishwa kwa kukosa idhini ya kuzungumza na waandishi wa habari, amesema treni hiyo bado imekwama kabla ya handaki lililozungukwa na milima.
Eneo ambalo treni hiyo imesimama ni eneo la milimani linalofanya iwe rahisi kwa wanamgambo kuwa na maficho na kupanga mashambulizi.