Wanamgambo wanane wanaoiunga mkono serikali wauawa Nigeria
28 Mei 2025Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, wanamgambo waliuawa wakati wakirejea kwenye mji mkuu wa jimbo hilo, Maiduguri, wakitokea eneo la Ziwa Chad, walikokuwa kwenye mapambano dhidi ya kundi moja la siasa kali lililovamia kambi ya kijeshi.
Katikati ya mwezi huu, wapiganaji wa kundi lijiitalo Dola la Kiislamu Jimbo la Afrika Magharibi, ISWAP, waliivamia kambi ya kijeshi mjini Marte, ambapo waliwauwa wanajeshi wanne kabla ya kuiteketeza kambi hiyo kwa moto.
Soma zaidi: Watu 30 wauawa Nigeria
ISWAP na kundi hasimu la Boko Haram wameendelea na mashambulizi yao kwenye majimbo ya Borno, Adamawa na Yobe kwa miezi kadhaa sasa.
Mzozo huo wa miaka 16 umeenea hadi nchi jirani za Cameroon, Chad na Niger, na kupelekea kuundwa kwa muungano wa kijeshi wa mataifa hayo kukabiliana na wapiganaji wa siasa kali.