RSF wadai kudungua ndege ya jeshi la Sudan
3 Aprili 2025Kwa mujibu wa video iliyochapishwa ambayo haijathibitika,wapiganaji wa RSF waliidungua ndege ya jeshi la Sudan aina ya Antonov kwenye eneo la kaskazini mwa Darfur siku ya Alhamisi. Hata hivyo hakuna tamko rasmi la jeshi la Sudan kufuatia tukio hilo.
Wapiganaji wa RSF wanadai kuwa walidungua ndege zilizotumiwa na jeshi awali ikiwemo moja ya usafiri iliyodondoshwa eneo hilohilo la Darfur mwezi wa Oktoba.
Soma pia:Wanamgambo wa RSF wawauwa watu 85 katika wiki moja
Mwanzoni mwa wiki, kiongozi wa kundi la RSF, Mohamed Hamdan Dagalo,alisisitiza kuwa vita kati yao na jeshi la serikali havijafikia kikomo na kwamba wapiganaji wake watarejea Khartoum hata baada ya kufurushwa.Ifahamike kuwa Darfur ni ngome ya wapiganaji wa RSF.
Vita hivyo vilivyoanza miaka miwili iliyopita vimewaacha mamilioni bila makaazi na maelfu kuuawa.
UN: Yachukizwa na mauaji ya kiholela Sudan
Kwa upande wake Umoja wa mataifa umechukizwa na mauaji ya kiholela ya raia wa kawaida wakati wa purukushani za kuwasukuma wapiganaji wa RSF kuiondoka Khartoum.
Mkuu wa shirika la kutetea haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa Volker Turk amesikitishwa sana na mauaji hayo imeeleza taarifa yake.Kauli hizo zinaungwa mkono na msemaji wa afisi ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya haki za binadamu,OHCHR, Seif Magango.
"Tumesikitishwa na ripoti za mauaji ya kiholela ya raia wa kawaida mjini Khartoum baada ya jeshi la Sudan kufanikiwa kuudhibiti mwishoni mwa Machi.Tunawasihi makamanda wa jeshi la serikali ya Sudan kuchukua hatua za dharura kutokomeza mauaji hayo yasiyokuwa na msingi.”
Duru zinaeleza kuwa kundi la wapiganaji wa RSF limewaua watu wasiopungua 85 katika kipindi cha wiki moja wakati wa mapambano ya kusini mwa Khartoum.
Soma pia:Kiongozi wa RSF athibitisha jeshi lake kuondoka Khartoum
Vita hivyo vilianza baada ya mvutano wa uongozi kutokea kati ya jeshi la serikali na wapiganaji wa RSF katika kipindi cha mpito cha kuupisha utawala wa kiraia.
Sudan imegawika mara mbili huku,jeshi likimiliki maeneo ya kaskazini na mashariki nao wapiganaji wa RSF wakidhibiti eneo la Darfur na lile la kusini.