Wanamgambo Sudan watangaza serikali hasimu
16 Aprili 2025Miaka miwili tangu kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan, Kikosi cha Wanamgambo cha Rapid Support Forces (RSF) kimetangaza kuunda serikali yake inayopingana na ile inayoungwa mkono na jeshi la taifa.
Tangazo hilo limekuja wakati Sudan ikiendelea kukabiliwa na mgogoro mkubwa wa kibinadamu uliosababisha vifo vya maelfu na kuwafurusha watu milioni 13 makwao, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.
Soma pia:Katibu Mkuu wa UN ataka usafirishaji wa silaha kuelekea Sudan usitishwe
Kiongozi wa RSF, Mohamed Hamdan Daglo, ametangaza kupitia Telegram kuanzishwa kwa "Serikali ya Amani na Umoja," ikidai kuwa ni muungano mpana unaoakisi matakwa ya wananchi.
Serikali hiyo inajengwa juu ya katiba ya mpito waliyoisaini na washirika wao mwezi Februari nchini Kenya, ambayo inajumuisha baraza la urais lenye wajumbe 15 kutoka kanda zote za nchi.
Wachambuzi wanaonya kuwa hatua hii inaweza kuifanya Sudan kugawanyika kabisa, hasa kwa kuzingatia nguvu kubwa ya RSF katika eneo la Darfur na ukosefu wa matarajio ya amani ya karibu.