Wanajeshi wengine wa Afrika Kusini wauawa mashariki Kongo
28 Januari 2025Habari kutokea Goma siku ya Jumanne (Januari 28), zilisema kuwa wanajeshi wengine wanne wa Afrika Kusini walikuwa wameuawa wakiwa kwenye mapambano na wapiganaji wa kundi la waasi la M23.
Shirika la utangazaji la Afrika Kusini (SABC) liliripoti kuhusu vifo hivyo, ambavyo viliongeza idadi ya wanajeshi wa nchi hiyo waliouawa mashariki mwa Kongo kwa siku za karibuni kufikia 14.
Soma zaidi: Hali mjini Goma bado ni tete: UN
Habari hizo zilithibitishwa na wizara ya ulinzi ya Afrika ya Kusini, ambayo kwenye taarifa yake ilisema licha ya maafa hayo, bado wanajeshi wao wangeliendelea kubakia kutekeleza jukumu lao.
Rais Cyrill Ramaphosa wa Afrika Kusini alizungumza na mwenzake wa Rwanda, Paul Kagame, kuhusiana na hali ya mashariki mwa Kongo, ambako waasi wa M23 wanaaminika kuungwa mkono na serikali ya Kigali.
Viongozi hao wawili walikubaliana haja ya usitishaji wa mapigano na kupunguza uhasama mashariki mwa Kongo.
ICG yataka usitishaji mapigano
Kundi la Mawasiliano ya Kimataifa kuhusu Maziwa Makuu, (ICG) linaloongozwa na Ujerumani limetowa wito wa kuachwa mara moja mapigano mashariki mwa Kongo, ikiwa ni siku chache tu baada ya waasi wa M23 kuutwaa mji wa Goma.
Taarifa iliyotolewa na kundi hilo siku ya Jumanne iliwataka marais wa Kongo na Rwanda kurejea kwenye meza ya mazungumzo.
Soma zaidi: Mpaka wa Kongo-Rwanda yafungwa baada ya waasi wa M23 kuiteka Goma
"Mamlaka na heshima ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo lazima iheshimiwe, pande zote za mzozo huo zisitishe mapigano kama zinavyotakiwa na makubaliano ya kusitisha vita yaliyosainiwa mwezi Agosti mjini Luanda, Angola." Ilisema sehemu ya taarifa ya ICG.
Siku ya Jumatano (Januari 29) kulitegemewa kufanyika mkutano kati ya viongozi hao ambao uliitishwa na mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rais William Ruto wa Kenya.
Lakini hakukuwa na uhakika endapo Kagame na Rais Felix Tshisekedi wa Kongo wangelihudhuria mkutano huo wa Nairobi.
Mapigano yaendelea Goma
Kwenyewe mjini Goma, kuliripotiwa mapigano ya hapa na pale kati ya waasi wa M23 na wanajeshi wa Kongo wanaoungwa mkono na kundi la vijana wajiitao Wazalendo.
Wakaazi wa huko walisema wamesikia milio kadhaa ya risasi na miripuko mikubwa asubuhi ya Jumanne, hasa karibu na uwanja wa ndege, ambapo ulikuwa bado uko mikononi mwa vikosi vya Umoja wa Mataifa na wanajeshi wa serikali.
Mkaazi mmoja wa mtaa wa Majengo ulio karibu na uwanja wa ndege, kaskazini mwa mji wa Goma, aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba ingawa hali ilikuwa shuwari usiku lakini kufika usiku wa manane risasi zilianza tena.
Soma zaidi: Serikali ya DRC yathibitisha uwepo wa jeshi la Rwanda huko Goma
"Nimesikia milio ya risasi kuanzia usiku huo wa manane hadi sasa kutokea karibu na uwanja wa ndege." Alisema bibi huyo.
Kwa ujumla, mapigano ya siku mbili (Jumatatu na Jumanne) yalikuwa yamepoteza maisha ya watu 17 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 370 kwa mujibu wa vyanzo vya hospitali, wakati wanajeshi wa Kongo wakijaribu kuwaondosha waasi wa M23 kutoka mji huo wa Goma.