Wanajeshi wa Uganda na Sudan Kusini washambuliana vikali
30 Julai 2025Ijapokuwa hadi sasa hakuna ushahidi wa ni nani aliyeanzisha mapigano hayo baina ya jeshi la Uganda na Sudan Kusini ambayo kihistoria ni washirika, jeshi la Sudan Kusini limethibitisha kutokea kwa mapigano hayo ambamo wanajeshi watano wa Sudan Kusini waliuawa. Uganda imekuwa na historia ya kuingilia ndani masuala ya Sudan Kusini na imekuwa mstari wa mbele kuiunga mkono serikali ya Rais Salvar Kiir kwa kumpa ulinzi na usalama wa karibu ikiwa ni pamoja na kupeleka kikosi maalum nchini Sudan Kusini mwezi Machi mwaka huu.
Mzozo wa Sudan unasambaa hadi Jamhuri ya Afrika ya Kati
Polisi katika kaunti ya Kajo Keji katika jimbo la Equatoria ya Kati imesema kwamba wanajeshi wawili wa jeshi la Sudan Kusini, maaskari magereza wawili na afisa wa polisi mmoja, jumla watano waliuawa na jeshi la Uganda wakati wa makabiliano hayo.
Taarifa hiyo ya polisi imemnukuu afisa mmoja wa jeshi la polisi nchini Sudan Kusini akisema kwamba jeshi la Uganda liliingia ndani ya eneo lao likiwa na silaha nzito na kuyalenga maeneo 19 ya kuendeshea operesheni zao za kijeshi.
Mmoja wa viongozi wa kaunti hiyo ambaye hakutaja jina lake amesema mapigano hayo yamesababisha idadi kubwa ya wananchi kuyahama makazi yao na hapa namnuku, ''mashambulizi ya jeshi la Uganda yamesababisha hasara kubwa ya watu kupoteza maisha na wengine kukimbilia vichakani, nyumba za ibada na majengo ya shule jirani'', mwisho wa kumnukuu.
Hakuna taarifa iliyokwishatolewa na jeshi la Uganda kuhusu mapigano hayo, lakini taarifa za awali zilisema kwamba kulikuwa na majeruhi kwa pande zote mbili. Shirika la habari la Reuters kwa upande mwingine limetangaza kwamba jeshi la Uganda kupitia msemaji wake meja Jenerali Felix Kulayigye amesema kwamba wanajeshi wa Sudan Kusini walivuka mpaka na kukita kambi katika eneo la Uganda na walipotakiwa kurudi nyuma walikataa na ndiyo ikasababisha jeshi la Uganda kutumia nguvu kuwarejesha nyuma.
Uganda ilituma kikosi chake nchini Sudan Kusini mwaka 2013 wakati nchi hiyo ilipoingia kwenye mapigano makali ya wenyewe kwa wenyewe miaka miwili tu baada ya kupata uhuru kutoka kwa Sudan mwaka 2011.
Upinzani wapuuza wito wa mazungumzo ya amani Sudan Kusini
Uganda kwa mara nyingine tena ilipeleka kikosi maalum nchini Sudan Kusini mwezi Machi mwaka huu baada ya Rais Salvar Kiir kutofautiana tena na makamu wake Dokta Riek Machar na hatimaye kumuweka katika kizuizi cha nyumbani. Hali hiyo imehatarisha mpango wa kugawana madaraka baina ya wawili hao na kusababisha mzozo kati ya jeshi na wanamgambo wa kabila la Nuer la Machar.
Hata hivyo, jeshi la Uganda limekuwa likishutumiwa kwa kutumia silaha za kemikali dhidi ya wanamgambo wa kabila la Nuer, kaskazini mashariki mwa Sudan Kusini. Uganda imekuwa ikikanusha shutuma hizo.