Pakistan na India zashambuliana huko Kashmir
25 Aprili 2025Uhusiano kati ya nchi hizo mbili umevurugika pakubwa hivi karibuni baada ya India kuishutumu Pakistan kwa kuunga mkono vitendo vya ugaidi vinavyoendeshwa ndani na nje ya maeneo ya mipakani, baada ya watu wenye silaha kushambulia na kuwaua raia 26 huko Pahalgam katika eneo la Kashmir lenye Waislamu wengi na ambalo limekuwa likizozaniwa kwa karibu robo karne.
Syed Ashfaq Gilani, afisa wa serikali huko Kashmir inayotawaliwa na Pakistan, ameliambia shirika la habari la AFP leo kwamba wanajeshi walishambuliana kwa risasi kwenye eneo la usalama linalotenganisha nchi hizo mbili, na kuongeza kuwa raia hawakulengwa na mashambulizi hayo. Jeshi la India kwa upande wake limethibitisha kutokea kwa mashambulizi madogo ambayo wamesema yalianzishwa na Pakistan na kusisitiza kuwa yalijibiwa ipasavyo.
Wito wa Umoja wa Mataifa kwa India na Pakistan
Umoja wa Mataifa kupitia msemaji wake Stephane Dujarric umeyatolea wito mataifa hayo mawili ambayo yanamiliki silaha za nyuklia kujizuia na kutoutanua mzozo huo:
"Tulilaani kwa uwazi shambulio la kigaidi lililotokea Jammu na Kashmir tarehe 22 mwezi huu, ambalo liliua idadi kubwa ya raia. Lakini tunatoa wito kwa serikali za Pakistan na India kujizuia na kuhakikisha kuwa hali ya sasa haizidi kuzorota. Tuna imani kwamba masuala yote kati ya nchi hizo mbili yanaweza na yanapaswa kutatuliwa kwa njia ya amani na ushirikiano wa kina."
Soma pia: Mzozo wazidi kufukuta kati ya India na Pakistan baada ya shambulio Kashmir
Waziri Mkuu wa India Narendra Modi ameapa kuwasaka na kuwawajibisha wale wote waliohusika na mauaji katika eneo maarufu la kitalii huko Pahalgam, akisema kuwa hata wale waliowasaidia watalipia gharama kubwa. Serikali ya Islamabad imekanusha kuhusika kwa vyovyote vile na shambulio hilo ikisisitiza kuwa majaribio ya kuihusisha Pakistan na shambulio la Pahalgam ni "ya kipuuzi" kwamba Pakistan iko tayari kujibu vikali hatua yoyote ya India.
Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif alisema wakati wa mkutano na Kamati ya Usalama ya Kitaifa na wakuu wa jeshi kwamba tishio lolote kwa uhuru na usalama wa watu wake litakabiliwa na hatua madhubuti.
(Vyanzo: Mashirika)