Wanajeshi wa Kimarekani washambuliwa tena Iraq
7 Desemba 2003Matangazo
BAGHDAD: Huko Iraq ya Kaskazini umeshambuliwa tena msafara wa magari ya wanajeshi wa Kimarekani. Mwanajeshi mmoja wa Kimarekani aliuawa na wengine kadha walijeruhiwa katika shambulio hilo mjini Mossul, waliarifu wanajeshi wa Kimarekani. Wakati akiendeleza ziara yake isiyotazamiwa nchini Iraq, Waziri wa Mambo ya Ulinzi wa Marekani Donald Rumsfeld alisema mjini Baghdad hii leo hana uhakika iwapo hivi sasa zimechomoza ishara za hali ya shwari tangu yapungue mashambulio dhidi ya wanajeshi wa Kimarekani mnamo wiki mbili za nyuma. Bwana Rumsfeld alisisitiza niya yake ya kutaka kukiongeza kiwango cha vikosi vya usalama vya Kiiraq kwa shabaha ya kuituliza hali ya usalama. Wakati huo huo Waziri huyo wa Mambo ya Ulinzi wa Marekani alisema anaunga mkono Iraq ikabidhiwe uhuru wake haraka iwezekanavyo.