Wanajeshi wa Afrika Kusini waingia Tanzania wakiondoka Kongo
5 Mei 2025Hayo yameelezwa na Mkuu wa Majeshi wa Afrika Kusini Jenerali Rudzani Maphwanya.
Jenerali huyo amesema chini mpango wa kuondoka kwa makundi ulioanza Aprili 29, wanajeshi wote waliokuwepo mashariki mwa Kongo wanasafirishwa kwa barabara kupitia Rwanda na kisha kuingia Tanzania, kabla ya kurejea Afrika Kusini.
Wanajeshi hao ni sehemu ya kikosi cha Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika, SADC, kilichotumwa Kongo mwezi Disemba mwaka 2023 kuwadhibiti waasi wa M23.
Jumuiya hiyo iliamua kujiondoa Kongo katikati mwa mwezi Machi baada ya M23 kuyakamata maeneo makubwa ya ardhi ya Kongo.
Maphwanya amesema tayari wanajeshi 57 wa Afrika Kusini wamewasili Tanzania na kundi jingine litaondoka Kongo wiki ijayo kwenda Tanzania kabla ya kusafirishwa kwa ndege kurejea nchini mwao.