Wanajeshi saba wa Israel wauwawa Gaza
25 Juni 2025Wanajeshi saba wa Israel wameuawa katika mripuko uliosababishwa na bomu la kutegwa ndani ya gari lao huko Khan Younis, Kusini mwa Ukanda wa Gaza.
Katika tukio jingine, wanajeshi kadhaa wa Israel waliuliwa na wengi kujeruhiwa baada ya wanamgambo wa tawi la Hamas la Qassam Brigade kuwavamia kwenye jengo moja huko Kusini mwa Gaza.Soma pia: Israel yashambulia makao makuu ya usalama wa ndani wa Iran
Matukio hayo mawili bado haijawa wazi ikiwa yanahusiana ingawa ripoti za shirika la habari la AP zinaonesha wanajeshi saba waliouliwa Khan Younis ni kutokana na mripuko uliosababishwa na bomu la kutegwa kwenye gari lao la kijeshi kwa mujibu wa maafisa wa Israel.
Tukio hilo limeripotiwa kufanyika jana Jumanne likitajwa kuwa shambulio baya zaidi dhidi ya wanajeshi wa Israel ndani ya Gaza.
Hukohuko Khan Younis mwanajeshi mmoja wa Israel alijeruhiwa vibaya baada ya kupigwa risasi. Waziri mkuu Benjamin Netanyahu ameiita siku ya leo kuwa ngumu mno kwa Israel kufuatia mauaji hayo.
Tawi la kijeshi la Hamas la Al-Qassam Brigade limeeleza kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Telegram, kwamba limevamia na kuwashambulia kwa risasi wanajeshi wa Israel waliokuwa ndani ya jengo moja la makaazi ya watu Kusini mwa Ukanda wa Gaza.
Lakini pia likasema baadhi ya wanajeshi wa Israel waliuwawa na wengine kujeruhiwa kwa kufyetuliwa makombora. Mashambulizi hayo yamekuja katikati ya matukio ya kuendelea kuuliwa kwa Wapalestina ndani ya Gaza ambapo hadi sasa idadi ya waliouwawa imefikia zaidi ya 56,000 kwa mujibu wa wizara ya afya ya Gaza.Soma pia: Israel yaendeleza mashambulizi Gaza
Zaidi ya wanajeshi 860 wa Israel wameuliwa na Waisrael 251 kutekwa na Hamas tangu vita hivyo vilipoanza Oktoba 7 mwaka 2023.
Hapo jana pia yalifanyika maziko ya mateka Yonatan Samerano ambaye mwili wake ulichukuliwa kutoka Gaza na kurudishwa Tel Aviv ambako familia yake na marafiki walikusanyika. Rais wa Israel Isaac Herzog aliyeshiriki maziko hayo alishadidia juu ya Israel kuendelea na vita hiyo ya Gaza.
''Hakuna mwisho na ushindi kamili wa vita hivi hadi tutakapowarudisha mateka wetu wote. Baadhi tuwarudisha makwao na wengine tuwape maziko ya heshima katika ardhi ya Israel. Kutoka mahala hapa patukufu na kipindi hiki cha majonzi natowa mwito kwa mateka wetu kwa kuwaambia, nchi nzima inawahitaji nyumbani. Taifa halitochoka na halitokaa kimya hadi nyote mtakaporejea nyumbani''
Soma pia: Wapalestina wasiopungua 20 wameuwawa wakisubiri misaada Ukanda wa GazaHivi leo afisa mmoja wa Palestina amesema wanajeshi wa Israel wamempiga risasi na kumuua mwanamke wa miaka 66 huko Jerusalem Mashariki.
Afisa huyo amesema jeshi la Israel lilivamia kambi ya wakimbizi ya Shuafat usiku wa kuamkia leo, na kumuua Zahia Obeidi, na kisha kuondoka na mwili wake,na kuikamata familia yake.Jeshi la polisi la Israel limesema linachunguza tukio hilo.
Na muda mfupi uliopita kundi la Hamas limesema juhudi za kufikia makubaliano ya amani Gaza zimepamba moto huku rais wa Marekani Donald Trump akisema anaamini hatua kubwa inapigwa kumaliza vita vya Gaza.