Wanajeshi 84, DRC wapandishwa kizimbani kwa tuhuma za mauaji
11 Februari 2025Matangazo
Wanajeshi hao wanatuhumiwa kwa kuvunja nyumba za raia katika vijiji kadhaa vya maeneo ya Kabare na Kalehe, jimboni Kivu Kusini mwishoni mwa juma. Mmoja wa mawakili wanaowawakilisha wahanga wa kiraia Pascal Mupenda, alisema kuwa wanajeshi hao wanadaiwa kuwabaka wanawake kadhaa na kuua takriban watu 12. Wanajeshi hao walioshtakiwa walifikishwa mbele ya mahakama ya kijeshi huko Bukavu, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kusini, siku ya Jumatatu. Kesi hiyo inajiri wakati waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda wakizidi kupata mafanikio Kivu Kusini baada ya kuuteka mji muhimu wa Goma katika jimbo jirani la Kivu Kaskazini.