Wanajeshi 5 wauwawa Tanganyika huko DRC
28 Aprili 2025Wanajeshi kwenye eneo hilo hujikuta wameyahatarisha maisha yao wakati wakiwalinda raia wa China, ambao wako huko kwa shughuli za kibiashara na uwekezaji, huku watekaji nao wakiwatumia raia hao wa kigeni kama mateka ili kupata pesa kwa urahisi.
Mauaji hayo yametokea Jumamosi katika msitu uliopo takribani kilomita 40 kutoka mjini Kalemie, ambapo watu wenye silaha wakivalia sare za kijeshi walivamia na kuwauwa wanajeshi hao kabla ya kutoweka na raia wa Kichina anayefanya kazi kwenye kampuni ya Great Lake Cement, kampuni ya kuchakata saruji jimboni Tanganyika.
Uvamizi kama huo ulifanyika mwaka 2024
Mratibu wa tarafa ya Kalemie, John Mutombe, amelaani mashambulizi hayo, akiapa kwamba serikali itawasaka wahalifu hao popote walipo. Ofisi ya mratibu huyo imeiambia DW kuwa ni mara ya tano sasa kwa visa kama hivyo kutokea katika maeneo hayo, ambapo hadi sasa wanajeshi tisa wameshauawa. Mika Omari ni msemaji wa ofisi hiyo.
"Mara kwa mara, Wachina ndio wamekuwa malengo ya wezi hao wenye silaha, kulingana na habari tulizonazo ni watu ambao wamevalia sare za kijeshi, hadi sasa haijulikani ni jeshi la kutokea wapi," alisema Omari.
Tukio kama hilo lilitokea mwaka jana ambapo wanajeshi wawili waliuawa kwa kupigwa risasi pia.
Kutokana na kutekwa mara kwa mara kwa wawekezaji kunawekea doa jimbo hili ambapo mashirika ya kiraia yanadai kuwa kuna mkono mrefu ndani ya matukio hayo. Mmoja wa wawakilishi wa mashirika hayo ni Byaesse Isa.
"Haiwezekani kila tukio linashuhudiwa eneo lile lile. Hiyo inatuonesha taswira kwamba kuna baadhi ya watu kwa namna moja au nyingine wanahusika na vitendo ambavyo vinaendelea kushuhudiwa sehemu hiyo," alisema Isa.
Jeshi lathibitisha kufariki wanajeshi wao
Hayo yanafanyika siku chache baada ya kampuni hiyo ya GLC kuwanyooshea kidole cha lawama wanajeshi kwa unyanyasaji na kuwapokonya vitu wafanyakazi wa kampuni hiyo.
Upande wao jeshi la Kongo jimboni Tanganyika limethibitisha vifo vya wanajeshi hao. John Monta ni afisa habari wa FARDC.
"Tumethibisha askari watano wa maji walipigwa risasi na kumpora hata mchaina ili wapate tu faranga, tuhuma za kutuhumu jeshi ni kwa sababu wanajeshi ndio wameshikilia silaha," alisema Monta.
Mara kadhaa watekaji hutumia mbinu hizo hizo kwa kutaka kulipwa maelfu ya dola za Kimarekani ili kuwaachilia mateka wanaowashikilia.