Tanzania yasema haitakubali kuchezewa shere na wanaharakati
20 Mei 2025Serikali ya Tanzania imeweka wazi sababu za kuwakamata na kuwarudisha makwao wanaharakati kutoka Kenya na Uganda waliokuwa wamefika jijini Dar es Salaam kushuhudia mwenendo wa kesi ya Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu. Tukio hilo limeibua mjadala mkubwa kuhusu uhuru wa mahakama, uhusiano wa kikanda na nafasi ya wanaharakati katika muktadha wa haki za binadamu Afrika Mashariki.
Akizungumza na wanahabari jijini Dodoma, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro, alisema wanaharakati hao walikamatwa kwa sababu hawakuwa na leseni za uwakili zinazowaruhusu kushiriki katika shughuli za kisheria nchini Tanzania. Aliongeza kuwa ujio wao ulikuwa na nia ya kuvunja sheria za nchi.
Watu waliokumbwa na hatua hiyo ni pamoja na mwanaharakati maarufu wa Kenya, Boniface Mwangi, na Agather Atuhaire kutoka Uganda, ambao walikamatwa na kuzuiliwa katika kituo cha polisi kati, Dar es Salaam, kabla ya kuachiwa na kurejeshwa makwao. Hali hiyo imejiri baada ya wanasiasa wengine kama Martha Karua na Jaji Mkuu Mstaafu wa Kenya, Willy Mutunga, kuzuiwa kuingia nchini punde tu walipotua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Huku wakirejeshwa nchini kwao, wanaharakati kutoka Kenya waliendesha kampeni mitandaoni wakilaani kitendo hicho na kuitaka serikali ya Tanzania kuwaachia huru Mwangi na Atuhaire. Miongoni mwa waliopaza sauti alikuwa Hussein Khalid, Mkurugenzi wa Vocal Africa, aliyesema kuwa haki haipaswi kuzuiwa mipakani.
Wanaharakati waandamana Kenya
Katika hatua ya mshikamano, wanaharakati kutoka Kongamano la Mapinduzi nchini Kenya walifanya maandamano na kutoa wito kwa serikali zote zinazohusika kuheshimu haki za binadamu, uhuru wa kujieleza na uhuru wa kushiriki katika masuala ya haki na uwajibikaji wa utawala.
Soma pia: Kenya yataka waliokamatwa Tanzania kuachiwa huru
Kwa upande mwingine, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi, alikiri kuwa yapo masharti ya kisheria kwa wageni, lakini akasisitiza kuwa kama hawajavunja sheria, basi waruhusiwe kufanya kile kilichowaleta nchini kwa mujibu wa haki za kimataifa.
Sakata hili limeibua maswali kuhusu jinsi nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zinavyoshughulikia masuala ya kisiasa yanayovuka mipaka, hasa pale ambapo haki za raia na uhuru wa kushiriki mijadala ya kisiasa vinapoguswa.
Tundu Lissu, ambaye ni mmoja wa wanasiasa mashuhuri wa upinzani Tanzania, ameendelea kuwa gumzo la kisiasa tangu kurejea nchini humo kwa ajili ya kushiriki shughuli za kisiasa na kesi yake inayohusu tuhuma za uchochezi na uhaini. Uwepo wa wageni waliokuja kufuatilia kesi hiyo ulionekana na baadhi ya maafisa kama tishio la kisiasa.
Soma pia: CHADEMA yapambana na msukosuko mpya wa kisiasa Tanzania
Huku mashirika ya kiraia na mashirika ya kimataifa ya kutetea haki yakifuatilia kwa karibu maendeleo haya, hatua ya Tanzania inaweza kuibua ukosoaji zaidi kuhusu utawala wa sheria na hali ya demokrasia nchini humo.
Kwa sasa, jicho la Afrika Mashariki limeelekezwa Tanzania, huku wananchi na watetezi wa haki wakijiuliza: Je, kufuatilia mwenendo wa kesi kwa nia ya uwazi ni kosa la jinai? Au kuna vuguvugu linalokuja dhidi ya sauti za upinzani?