Wanaharakati wa Kenya na Uganda waishtaki Tanzania EACJ
19 Julai 2025Mkenya Boniface Mwangi na Agather Atuhaire wa Uganda, waliwasilisha kesi hiyo jana Ijumaa wakidai kuwa walifanyiwa unyama huo walipozuiliwa jijini Dar es Salaam kati ya Mei 19 na 23 mwaka huu, walipokamatwa wakijaribu kuhudhuria kesi ya kiongozi mkuu wa upinzani nchini Tanzania Chadema Tundu Lissu, ambaye anakabiliwa na kesi ya uhaini.
Wanaharakati hao pamoja na walalamikaji wengine saba wamesema katika tamko lao la pamoja kuwa wanadai fidia kwa "ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na vitendo vya utekaji, kuteswa, kuwekwa kizuizini kiholela na kufukuzwa nchini kinyume cha sheria" wakisisitiza kuwa hayo yalitekelezwa na mawakala wa serikali ya Tanzania.
Wameendelea kuwa serikali za Kenya na Uganda zilishindwa katika wajibu wao wa kisheria wa kuwalinda raia wao kwa kutumia njia zote za kidiplomasia ili waweze kurejea salama katika nchi zao. Tanzania na Kenya hazijazungumzia chochote juu ya kesi hiyo.