Wanaharakati wa Kenya bado wanazuiliwa Tanzania
21 Mei 2025Yupo wapi Boniface Mwangi na Agatha Atuhaire? Hayo ndiyo maswali yanayoulizwa na wanafamilia, raia wa Kenya na wanaharakati wa Tanzania, Kenya na Uganda, baada ya wanaharakati hao wawili kutorejea nchini mwao kama ilivyotarajiwa. Hata hivyo, majibu yaliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Musalia Mudavadi ni haya.
"Yupo tanzania, ninawasiliana na mamlaka za kenya huko, anashikiliwa na mamlaka na tunatarajia ataachiliwa," alisema Musalia Mudavadi.
Wanaharakati hawa walishikiliwa na polisi mei 19 wakiwa hapa nchini ambako walifika kwa ajili ya kufuatilia mwenendo wa kesi ya uhaini inayomkabili, Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, CHADEMA, Tundu Lissu.
Wanaharakati wazuiliwa Tanzania: Sakata la kesi ya Tundu Lissu lazua mjadala mpana
Kwa mujibu wa mawakili waliokuwa wakiwapa msaada wa kisheria, jana Mwangi na Atuhaire waliachiwa na kupelekwa uwanja wa ndege wa Julius Nyerere DSM kwa ajili ya kurejeshwa katika nchi zao. Hata hivyo mke wa Mwangi, Njeri Mwangi, alilalamikia mamlaka za Tanzania kwa kushindwa kutoa taarifa za alipo mume wake na sababu za kumshikilia.
"Tunataka kujua Mwangi yupo wapi, mpaka sasa hajafika Hapa Kenya. mimi kama mke nina haki ya kutaka kujua alipo mume wangu, tujue na sababu za kumshikilia, Tunataka uhakika wa maisha yake na sababu za kumshikilia mpaka sasa," aliongeza kusema Njeri.
Mienendo ya waliokamatwa haijulikani
Awali DW ilipozungumza na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Tanzania, LHRC nao pia hawakuwa na taarifa zozote kuhusu walipo wanaharakati hao.
Hata hivyo, juhudi za kulipata jeshi la polisi ama uhamiaji hazikufua dafu baada ya simu zao kutopokelewa.
Wakati haya yote yakijiri serikali ya Tanzania kupitia Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa imetoa ufafanuzi kuhusu kudukuliwa kwa baadhi ya akaunti za mitandao ya kijamii ya serikali.
Samia: Hatutaki kuingiliwa mambo yetu ya ndani
"Zile taratibu zao za kiusalama zilikuwa si thabiti na kusababisha akaunti zao kuingiliwa, mitandao hiyo kwa sasa ipo salama," alisema Silaa.
Jana akaunti ya X ya Jeshi la Polisi ilidukuliwa kwa saa kadhaa na kuzua taharuki na baadaye jeshi hilo lilitoa taarifa ya kuwasaka waliofanya uhalifu wa kimtandao.