Wanaharakati Uganda washinikiza Besigye aachiwe
18 Februari 2025Baadhi ya waandamanaji katika mji wa Mbarara kusini magharibi mwa Uganda wamekuwa wakijaribu kuandamana na baadae kukamatwa na polisi.
Kwa sasa vyombo vya usalama vimekaa chonjo kufuatia kufukuta kwa maandamano hayo ya kudai kuachiwa kwa mkosoaji wa siku nyingi wa utawala wa Rais Yoweri Museveni.
Soma: Uganda: Besigye kuhukumiwa katika mahakama ya kiraia
Huku kamata kamata zikifanyika dhidi ya vijikundi vya wanadamanaji, viongozi wa vyama vya upinzani wamekutana na kutoa makataa ya saa 48 kwa utawala kumwachia Dkt Kizza Besigye na wafungwa wengine wa kisiasa.
Kwa mtazamo wao, baada ya mahakama ya juu kufutilia mbali uamuzi wa korti ya kijeshi, mwanasiasa huyo na wengine wanazuiliwa kinyume na katiba ya nchi.
Rais wa chama kikuu cha upinzani Robert Kyagulanyi ametoa tamko kwa niaba ya wenzake baada ya kikao chao hapo jana. "Sisi kama upinzani tumetoa ilani ya saa 48 Besigye na wenzake waachiwe la sivyo tutangaza kitakachofuata".
Kwengineko makundi ya asasi za kiraia yameishutumu serikali kwa kuendelea kukiuka haki za binadamu za watu wanaowataja kuwa wafungwa wa kisiasa.
Tangu kukamatwa kwa Dkt Besigye katika mtaa mmoja wa Nairobi mwezi Novemba mwaka uliopita, wanaharakati mbalimbali wameendelea kuishutumu serikali ya Kenya kwa kujihusisha na masuala ya kukandamiza haki za binadamu za raia wa Uganda.
Wanaharakati hao sasa wanaitaka Kenya kutoa tamko rasmi la kuirai serikali ya Uganda kumwachia Dkt Besigye kwani kukamatwa kwake kwenye ardhi yao ilikuwa kinyume na sheria. Bashira Nantogo ni mmoja kati ya wanaharakati hao na amesema kwamba "utawala wa Kenya ndiyo chanzo cha haya yote wanatakiwa kuhusika katika harakati hizi za kumwachia Dkt Besigye".
Huku raia mbalimbali wa Uganda walioko Ughaibuni wakiendesha maandamano kuhusiana na suala hilo, katibu mkuu wa Bunge la Jumuiya Ya Madola Patricia Scott ametoa taarifa ya rai kwa serikali ya Uganda iheshimu haki za binadamu na utawala wa kisheria na kidemokrasia.Korti ya kijeshi Uganda yasikiliza tena kesi ya Besigye
Ameelezea masikitiko yake kuwa kama mwanachama wa jumuiya hiyo, vitendo vya serikali ya Uganda vimeenda kinyume na maazimio na maadali ya jumuiya hiyo.
Bunge la Uganda linatarajiwa kujadili kuachiwa kwa Besigye na wafungwa wengine wa kisiasa. Hii ni baada ya kundi la wabunge kukusanya saini wakitaka suala hilo lishughulikiwe kwa dharura la sivyo ghadhabu za raia zitazidi kuleta mashaka na wasiwasi.