Wanahabari wauawa Gaza kufuatia mashambulizi ya Israel
25 Agosti 2025Mashambulizi ya Israel katika hospitali ya al Nasser huko Gaza leo Jumatatu yamesababisha vifo vya watu wasiopungua 15 wakiwemo waandishi wa habari watatu.
Mpiga picha Hussam al-Masri, mmoja wa waandishi wa habari waliouawa alikuwa ameajiriwa na shirika la habari la Reuters.
Mwandishi wa habari mwingine aliyeuawa ni Mohammed Salama wa shirika la utangazaji la Al Jazeera. Siku ya Jumapili, mpigapicha mwingine wa kituo cha Televisheni cha Palestina Khaled al-Madhoun aliuawa kwa kupigwa risasi karibu na kivuko cha Zikim.
Jeshi la Israel na Ofisi ya Waziri Mkuu hawajazungumza chochote kuhusiana na mashambulizi hayo lakini, Chama cha Waandishi wa Habari wa Palestina kimeeleza kusikitishwa na matukio hayo ya kuwalenga wanahabari kikisema kwamba hiyo ni "kampeni inayoendelea ya Israel dhidi ya waandishi wa habari na yenye lengo la kunyamazisha simulizi za Wapalestina."
Shadi Al-Arabi ni raia wa Palestina akielezea madhila wanayopitia katika mji wa Gaza: " Nimesalimika kutoka kwenye mashambulizi ya kijeshi na milio ya risasi nzito, kumekuwa na makabiliano makali pande zote. Hapa, hatuwezi kukaa kwenye mahema au nyumba zetu. Na sasa tunateseka hata kupata chakula na maji."
Shinikizo linaloikabili serikali ya Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na serikali yake wanakabiliwa na shinikizo la ndani na hata kimataifa ili kufikia haraka makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza ambayo pia yatawezesha kuachiliwa kwa mateka wa Israel ambao bado wako mikononi mwa kundi la Hamas.
Mkuu wa majeshi wa Israel Eyal Zamir ametahadharisha juu ya mpango wa kuchukua udhibiti wa mji wa Gaza akimtaka Netanyahu kufikia makubaliano haraka.
Wanachama wa siasa kali za mrengo wa kulia wanaounda serikali ya mseto ya Netanyahu wamekuwa wakitishia mara kadhaa kujiondoa kwenye serikali ya mseto ikiwa kutafikiwa makubaliano na Hamas, jambo ambalo linaweza kupelekea kuvunjika kwa serikali ya Netanyahu.
Matukio mengine kuhusu Yemen na Lebanon
Ama katika maeneo mengine huko Mashariki ya Kati, Israel iliushambulia vikali mji mkuu wa Yemen , Sanaa hapo jana na kusababisha vifo vya watu sita huku wengine 86 wakijeruhiwa.
Kampuni kubwa ya mafuta ya Asar na kituo cha kuzalisha umeme cha Hizaz viliharibiwa na mashambulizi hayo ya kulipiza kisasi dhidi ya Wahouthi ambao awali walifyetua makombora kuelekea Israel.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema wanajeshi wa Israel wanaweza kuanza kuondoka katika maeneo wanayoshikilia kusini mwa Lebanon baada ya "uamuzi muhimu" wa serikali mjini Beirut iliyochukuliwa mapema mwezi huu ya kuamua kuwapokonya silaha mwanamgambo wa kundi la Hezbollah kufikia mwishoni mwa mwaka 2025.
//AP, DPA, Reuters, AFP